Home Habari za michezo SIKU CHACHE BAADA YA KUONA MAZOEZI YA MBRAZILI…KAPOMBE AVUNJA UKIMYA SIMBA…

SIKU CHACHE BAADA YA KUONA MAZOEZI YA MBRAZILI…KAPOMBE AVUNJA UKIMYA SIMBA…

Habari za Simba SC

Beki Mkongwe wa Simba, Shomari Kapombe, ametoa ahadi nzito mbele ya kocha mpya wa timu hiyo, Mbrazil Robertinho Oliveira kuwa watahakikisha wanashinda kila mchezo uliopo mbele yao wa Ligi Kuu na kimataifa ili kutimiza malengo yao na kocha.

Simba imeweka kambi ya wiki moja Dubai, Falme za Kiarabu, ikijiandaa na Ligi Kuu, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo pia ni wakati maalum kwa Robertinho kuwasoma wachezaji wake vema baada ya kujiunga na timu hiyo mapema mwezi huu.

Akizungumza kutokea Dubai, Kapombe alisema wanahitaji kuungana pamoja kutimiza malengo yao na ya kocha kwa kuhakikisha wanajituma ipasavyo ili kuweza kushinda kila mchezo ulio mbele yao.

“Tunashukuru viongozi kwa kuweza kutufikisha hapa, ‘facility’ (sehemu ama vifaa) zote zinaturuhusu kufanya mazoezi kwa bidii, wachezaji tupo vizuri na mwalimu amezidi kutupa madini yake yatakayotusaidia katika ligi na kimataifa.

“Kambi hii ni nzuri kwetu kwani imetuweka pamoja baada ya kuwa katika makundi mawili wengine walikuwa kwenye michuano ya Mapinduzi na wengine mapumziko, hivyo ni kambi sahihi inayotufanya tuwe karibu na mwalimu ambayo inamsaidia kujua tabia ya kila mchezaji na kujua anahitaji nini hivyo itatusaidia.

“Mazoezi anayotoa mwalimu ni ya kiwango cha juu sana kila mchezaji anajitolea kwa kujituma, pia mwalimu kuna vitu ametueleza kama malengo yake na vitu vizuri ameviona kwetu atatusaidia, kocha amesema Simba ni timu kubwa yenye malengo, hivyo tupambane kwani amekuja kushinda.

“Hivyo sisi kama wachezaji tutajiandaa kushinda katika kila mechi ili tumsaidie mwalimu kutimiza malengo, hivyo inatupa changamoto ya kushinda kila mchezo ulio mbele yetu,” alisema na kuongeza;

“Mwalimu ametuelezea malengo yake na mafanikio aliyoyapata alipotoka, hivyo ametupa changamoto na chachu kwetu wachezaji ya kupambana.”

Jaribio la kwanza la Robertinho kwenye mechi za mashindano akiwa na Simba litakuwa mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumanne ijayo kabla ya kuifuata Dodoma Jiji Januari 22 na kisha kurejea Dar es Salaam kuikaribisha Singida Big Stars Februari 3, mwaka huu.

Baada ya mechi hiyo, ataiongoza Simba kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini nchini Guinea kuvaana na wenyeji wao, Horoya AC

SOMA NA HII  MRITHI WA LUIS AKUBALI KUTUA SIMBA