Home Habari za michezo BAADA YA MANGUNGU KUSHINDA TENA SIMBA…HAYA HAPA MAMBO 4 PASUA KICHWA YANAYOMKABILI…

BAADA YA MANGUNGU KUSHINDA TENA SIMBA…HAYA HAPA MAMBO 4 PASUA KICHWA YANAYOMKABILI…

Viongozi waliochaguliwa Simba SC

BAADA ya kutetea uenyekiti wa klabu ya Simba katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika juzi katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Murtaza Mangungu na vigogo wenzie wanakabiliwa na vibarua vinne ambavyo wanapaswa kuvifanyia kazi.

Mitihani hiyo inayomkabili Mangungu ni mpasuko uliopo ndani ya klabu hiyo, mabadiliko ya katiba, mchakato wa usajili wa wanachama na mashabiki pamoja na ushindani wa mataji katika mashindano mbalimbali.

Mangungu aliibuka mshindi katika uchaguzi dhidi ya Wakili Moses Kaluwa baada ya kupata kura 1,311 huku mshindani wake akipata kura 1,045.

Katika uchaguzi huo ambao ulimrudisha Mangungu madarakani wanachama watano wa Simba walichaguliwa katika nafasi za ujumbe wa bodi ya wakurugenzi ambao ni Dk Seif Ramadhani Muba, Asha Baraka, Issa Masoud Iddi, Rodney Makamba Chiduo na Seleman Harubu Said.

MPASUKO WA KLABU

Unaweza kuwa miongoni mwa chaguzi za Simba ambazo zilileta mgawanyiko mkubwa ndani ya klabu hiyo kuanzia wakati wa kampeni, muda wa uchaguzi na hata baada ya washindi wa nafasi tofauti kutangazwa.

Kuanzia kwa vigogo wa timu hiyo, mashabiki hadi wanachama waligawana baina ya wagombea wa uenyekiti na hilo lilidhihirishwa na kauli za vijembe, tambo, kejeli na kashfa ambazo ziliitolewa na wapambe na hata wagombea wenyewe jambo ambalo ni wazi liacha makovu na linapaswa kushughulikiwa kwa haraka.

Mpasuko mkubwa ulikuwa katika kundi maarufu la marafiki wa Simba ‘Friends of Simba?? ambalo baadhi ya wanachama wake ni viongozi ambapo kundi kubwa lilionekana kumuunga mkono Kaluwa huku wachache wakimsapoti Mangungu.

Kampeni zilitawaliwa na mashambulizi binafsi kwa wagombea badala ya hoja na hilo lilimfanya mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Boniface Lihamwike kuwaonya wagombea na wapambe kufanya kampeni za kistaarabu vinginevyo wangechukuliwa hatua.

Baada ya matokeo kutangazwa, kumekuwa na kundi ambalo limeonekana kutokukubaliana nayo lakini pia kuna lile lililokubaliana nayo huku likiendelea kukejeli wale walioshindwa.

Hii haitengenezi taswira nzuri Simba ikiwa uongozi hautashughulikia kwa haraka kutafuta suluhu ingawa Mangungu na Wakili Kaluwa wote wameonekana kuzungumzia suala la kudumisha umoja baada ya uchaguzi.

“Nimekuwa dissatisfied (sijakubaliana) na matokeo sikusaini matokeo lakini ombi langu kwenu, Simba ni kubwa kuliko uchaguzi. Simba ni kubwa kuliko sisi wote. Uchaguzi umekwisha kama kulikuwa na makundi makundi, yavunjike na kusambaratika, tuijenge Simba yetu. Tuna jukumu kubwa la kuijenga Simba, tunaipenda Simba hatupendi watu. Kwa maana hiyo ndugu zangu mimI kama Moses Kaluwa nitawapa ushirikiano viongozi. Yale niliyokuwa nayahubiri naamini watayatekeleza kama ni upungufu ila niwatakie kila la heri katika maisha yao ya uongozi,” alisema Kaluwa.

Mangungu alisema yanapaswa kusahauliwa.

“Mchakato umekwisha na yale ambayo yalitokea wakati wa mchakato basi yawe yamekwisha hii leo. Kila mmoja alikuwa na watu. Nashauri na kuwaomba sana wale ambao mliokuwa mnaniunga mkono msitumie nafasi hiyo kuwabeza wenzetu kwa sababu huu ni mchakato wa kidemokrasia,” alisema.

KILIO CHA KATIBA

Katiba ya sasa haimpi mamlaka makubwa mwenyekiti wa upande wa wanachama kwenye bodi ya wakurugenzi na badala yake mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ndiye ana mamlaka makubwa ya kuongoza na kusimamia timu.

Hiyo inatokea wakati ambao katiba hiyohiyo inabainisha kuwa wanachama wanamiliki asilimia 51 za hisa huku upande wa mwekezaji akimiliki 49.

Mangungu kwa nafasi yake anapaswa kupigania nguvu ya upande wake kwa vile ndio unamiliki asilimia nyingi za hisa na hilo linapaswa kurekebishwa kupitia katiba.

Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali ni miongoni mwa watu ndani ya Simba ambao hawaridhishwi na baadhi ya vipengele vya katiba na hata katika mikutano ya kampeni alisisitiza viongozi watakaochaguliwa kuhakikisha wanashughulikia mabadiliko ya katiba ili iwe na nguvu kwa wanachama.

USAJILI WA WANACHAMA

Awali Simba ilianzisha mchakato wa kusajili wanachama ambao kwa sasa watajulikana kama wanahisa ambao baadaye kila mmoja atakuwa na umiliki wa hisa za klabu hiyo jambo ambalo litakuwa na manufaa kwao na kwa klabu hasa katika suala zima la kiuchumi.

Ni mchakato ambao ungeweza kuipatia Simba kiasi kikubwa cha fedha lakini ghafla ukasimama na kwa sasa unaonekana kama umekufa kifo cha kawaida.

Lipo kundi kubwa la mashabiki wa Simba ambalo linatamani kuwa wanachama wa klabu hiyo lakini wapo wale wa zamani ambao wanatamani kuona wapo kwenye mfumo rasmi wa kutambulika ndani ya klabu yao.

MATAJI

Katika msimu uliopita, Simba ilipoteza mataji mawili iliyokuwa ikiyashikilia ambayo ni Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam lakini katika msimu huu pia wameachwa kwa tofauti ya pointi sita na watani zao Yanga kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu huku zikibakia raundi tisa tu msimu umalizike.

SOMA NA HII  IMEFICHUKA...LAKI MBILI TU ZAMPELEKA MSUVA YANGA..BOCCO KUMBE BADO WAMO..MASTAA WATEGEANA SIMBA..