Kaimu Kocha Mkuu wa Coastal Union, Joseph Lazaro amesema kitendo cha kuondolewa na Simba katika michuano ya Kombe la Azam (ASFC), imekuwa ni ahueni kwao kwani kwa sasa akili zao zitatulia upande mmoja tu wa Ligi Kuu Bara.
Coastal iliondoshwa na Simba kwenye hatua ya 32 bora baada ya kupoteza bao 1-0, mchezo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa licha ya miamba hiyo kufanya vizuri msimu uliopita ilipofika fainali na kufungwa na Yanga.
“Kwa hali yetu kiukweli kutolewa na Simba imetufanya tuweke nguvu katika ligi kwa sababu hatuko sehemu zuri na ukiangalia kwa jinsi ratiba ilivyo ingezidi kutupoteza kucheza huku na huku,” alisema Lazaro.
“Tunahitaji kubaki katika ligi msimu ujao na hilo tutalifanikisha kwa kuwekeza nguvu upande mmoja, tunajua tuko chini mwa msimamo hivyo lazima michezo yetu yote nane iliyobaki tuicheze kwa umakini na kwa tahadhari.”
Beki wa kikosi hicho, Emery Nimubona alisema: “Muda mwingine kupoteza mchezo inatokea tu kwa bahati mbaya na sio kwamba tunacheza vibaya, ukiangalia hata mchezo wetu na Simba tumecheza vizuri na tulionyesha upinzani mkali hivyo ni matokeo tu ya mpira wa miguu.”
Coastal ipo katika nafasi ya 12 ikiwa imecheza michezo 22, imeshinda michezo minne tu na kutoka sare saba huku ikiwa imepoteza michezo 11 kwenye ligi hiyo.
Mechi ijayo Coastal ni dhidi ya Mbeya City Jijini Tanga Februari 18 kabla ya kukiwasha na Prisons na Singida zote kwenye Uwanja huohuo.
I’m