Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amekiri Horoya ya Guinea iliwazidi akili kwenye mchezo wa juzi uliopigwa mjini Conakry, lakini akasema anapanga jeshi lake kwa mechi ijayo dhidi ya Raja Casablanca akifurahia kumtumia kiungo Saido Ntibazonkiza.
Saido hakusafiri na timu hiyo kutokana na kuwa majeruhi na kumlazimisha Mbrazili huyo juzi kuwaanzisha viungo wakabaji watatu kwa mpigo, Ismael Sawadogo, Sadio Kanoute na Mzamiru Yasin ambao bado walishindwa kuwamudu viungo wa timu wenyeji na Robertinho alifichua siri.
Alisema kikosi cha timu hiyo kililazimika kucheza kilivyocheza kwa kuheshimu wapinzani wao na hata matokeo hayo kwake ni nafuu kuliko kama angeamua kufunguka kama itakavyocheza nyumbani dhidi ya Raja ambapo amefichua atamtumia Saido kuwazima waarabu.
Robertinho alisema baada ya kuwaelekeza kipindi cha pili walicheza vizuri ikiwemo kutengeneza nafasi zaidi ya mbili za kufunga mabao tena zikiwa ndani ya boksi ila umakini mdogo kwa wachezaji ulichangia kupoteza kwa kushindwa kuzitumia kubadili kuwa mabao.
Alisema hilo limeisha tayari ila kama benchi la ufundi wanakwenda kulifanyia kazi ili kubadilika kwenye mchezo unafuata dhidi ya Raja Casablanca ambao anaimani kubwa watakwenda kushinda.
“Ukiangalia mechi ugenini kuna wakati tulicheza kwa kujilinda ikiwemo kuanza na viungo watatu wenye asili ya kuzuia ila hilo mchezo wa Raja Casablanca wala halitakuwepo,” alisema Robertinho na kuongeza;
“Mechi ya nyumbani kwenye dakika nyingi za mchezo tutacheza kwa kushambulia zaidi na kupeleka mashambulizi ya mengi ya mara kwa mara lengo likiwa ni kupata ushindi wa kwanza na hilo nikuhakikishie linawezekana kulingana na kikosi changu kilivyo,”
“Hata aina ya kikosi pamoja na mbinu tulizoanza nazo huku ugenini ukifuatilia mechi ya Raja kuna badaliko sahemu mbalimbali utayaona na lengo likiwa ni kupata ushindi ili kuwa kwenye mazingira mazuri.
“Kuna mchezaji muhimu kama, Saido Ntibazonkiza alikosekana ugenini kama atakuwa fiti mchezo dhidi ya Raja atapata nafasi ya kucheza kutokana na uwezo wake wa kufunga, kutoa pasi za mwisho mzuri kwenye kushambulia akiunganisha nguvu na wachezaji wengine naamini tutakuwa bora za ya mchezo wa kwanza.”
Katika hatua nyingine Robertinho alisema wachezaji na benchi la ufundi wote kwa pamoja wameangalia mechi ya wapinzani wao Raja dhidi ya Vipers na kuona vitu vingi vya kiufundi na wanakwenda kuvifanyia kazi.
“Ili kufanikisha yote hayo mapema tumeanza maandalizi ya mchezo wa nyumbani nimewaeleza wachezaji wangu tunatakiwa kuyafanya kwa umakini mkubwa na kwenda kuyatekeleza vizuri kiwanjani siku ya mechi,” alisema Robertinho na kuongeza; “Bado tunanafasi ya kufuzu hatua inayofuata kama malengo yetu yalivyo na hilo mbona linawezekana licha ya kupoteza mchezo huu wa kwanza ugenini.”