Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika Simba wako ugenini mbele ya wenyeji wao Vipers ya Uganda lakini mchezo huo mbali ya kuamua hatma za timu zote kusaka matuamini ya kusonga mbele pia itakuwa na uamuzi juu ya makocha wa timu zote.
Simba inahitaji matokeo ya ushindi kufufua matuamini yao ya kusonga mbele baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza matokeo ambayo yamewafanya kushika mkia katika kundi lao C.
Wekundu hao endapo wataambulia sare watajiweka katika nafasi ngumu lakini mashabiki wakipoteza watajiharibia zaidi na kufuta matuamini yao.
Wenyeji wao Vipers SC wao wanahitaji ushindi wa kwanza baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kisha kulazimishwa suluhu nyumbani na Horoya AC ya Guinea, matokeo ambayo yamewafanya kusalia nafasi ya tatu katika msimamo huo.
Mbali na mawindo hayo matokeo ya mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa St Mary’s uliopo eneo la Kitende, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 15,000 pia utaamua hatma ya makocha wa timu zote mbili.
Simba inayofundishwa na kocha wa zamani wa Vipers Robert Oliveira ‘Robertinho’ haijashinda mchezo wa CAF tangu Mbrazil huyo achukue timu kutoka kwa msaidizi wake mzawa Juma Mgunda ‘Guardiola Mnene’.
Robertinho alipoteza mbele ya Horoya AC (1-0), kisha kupoteza vibaya nyumbani dhidi ya vinara wa kundi lao Raja Athletic Club (0-3) huku mechi ya Ligi nyumbani akilazimisha sare ya bao 1-1 mbele ya Azam.
Matokeo hayo yameiweka katika presha kubwa ajira ya Robertinho na kama akipoteza mbele ya Vipers leo huenda akajiweka katika mazingira magumu kufuatia mashabiki wa timu yake kutilia shaka uwezo wake wa kuipa mafanikio timu hiyo.
Hali kama ya Robertinho pia ipo kwa mrithi wake pale Vipers Beto Bianchi ambaye naye anatokea kulekule Brazil ambapo katika m chi tatu zilizopita timu yake haijafunga bao lolote.
Vipers ilipoteza vibaya kwa mabao 5-0 ugenini dhidi ya Raja kisha kulazimishwa suluhu ya 0-0 dhidi ya Horoya nyumbani katika mchezo ambao timu yake ilipoteza nafasi nyingi.
Suluhu hiyo ikamfuata pia mechi ya Ligi wakilazimishwa suluhu dhidi ya Wakiso Giants, na kama akipoteza leo tayari vyombo vya habari mbalimbali kutoka Uganda vimeripoti leo kwamba Bianchi anaweza kupoteza kazi yake endapo atakosa matokeo mazuri kwenye mchezo huo dhidi ya Simba.
Timu zote zinazosubiri dakika 90 za leo kuona kama ipi itaanza kushangilia bao lao la kwanza kwenye mechi za Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kucheza mechi mbili zikitoka bila kufunga.