Roberto Oliveira ‘Robertinho’, Kocha Mkuu wa Simba, amesema wamemaliza kazi ya kuikabili Vipers mapema kwa kuwapa mbinu wachezaji wake na kupanga kikosi bora kitakachotoa matokeo mazuri.
Leo Jumanne, Simba inatarajiwa kumenyana na Vipers ikiwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi C ukichezwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
Akizungumza nasi, Robertinho alisema kazi ya kuikabili Vipers imekamilika, hivyo ni muda tu wa mchezo ufike ili vijana wake kuonesha uwezo wao.
“Mpango wetu kwa ajili ya mchezo wa kesho (leo) umekamilika, tunajua kwamba utakuwa mchezo mgumu dhidi ya wapinzani wetu hao.
“Malengo yetu ni kufanya vizuri na ninafurahi kuona namna ambavyo wachezaji wanafanya mazoezi wakiwa na furaha huku kila mmoja akiwa tayari kwa mchezo.
“Tayari nimeshapata kikosi cha kwanza kwa ajili ya mchezo dhidi ya Vipers, lakini kwa sasa sitakiweka wazi mpaka muda utakapofika.
“Hali ya kujiamini imezidi kuongezeka, hii ni nzuri kwetu, kupoteza mbele ya Raja Casablanca tukiwa nyumbani, hilo tumesahau na sasa ni muda wa kuwatazama wapinzani wetu Vipers kwani mchezo wa mpira sio kile kilichopita bali kilichopo mbele yetu.
“Tuna wachezaji wazuri ndani ya Simba, wenye ubora na vipaji ikiwa ni pamoja na Shomari Kapombe, nina furaha na wachezaji wote kwani wanacheza kwa ushirikiano na kufanya program zote, wapinzani wetu tunawaheshimu.
“Hatua kwa hatua tunazidi kuimarisha kikosi katika kila sekta kuanzia safu ya ulinzi na ushambuliaji, tunahitaji kufunga mabao ili kushinda mechi,” alisema Oliveira.
Shomari Kapombe, beki wa Simba, alisema: “Tumejiandaa kufanya vizuri, hicho ni kitu tunachokipenda. Tunajua Vipers mbinu yao kubwa ni kushambulia kwa kushtukiza, mwalimu ametuandaa katika mbinu za nje na ndani ya uwanja.
“Tumejiandaa kwa ajili ya mechi zote na malengo ni kuona tunatinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.”
VIPERS KUMKOSA KARISA
Wakati huohuo, nyota mgumu wa Vipers, Milton Karisa, kuna hatihati akaukosa mchezo wa leo dhidi ya Simba baada ya kocha wake, Roberto Bianchi kusema alipata maumivu mechi iliyopita.
“Mechi iliyopita tulipoteza na sasa kimahesabu kuna uwezekano wa kupata ushindi kwani mchezo uliopita dhidi yao tulicheza vizuri na kupata nafasi nyingi zaidi yao, labda uzoefu wa wachezaji wa Simba uliwafanya kupata matokeo mazuri, sasa mchezo huu ni muhimu.
“Ligi ya Mabingwa Afrika kinachoangaliwa ni makosa, ukifanya inakuwa gharama kwako, ninaamini tutakuwa na mchezo mzuri zaidi ya ilivyokuwa Uganda.
“Tumekuja Tanzania kama ambavyo Simba walikuja Uganda, sasa nasi tuna kazi ya kupata pointi tatu. Bado tuna nafasi kimahesabu, tunapaswa kuwa makini dhidi ya Simba.
“Tutamkosa Karisa, lakini wapo wachezaji wengine watakaocheza nafasi yake, yeye alipata maumivu katika mchezo uliopita,” alisema kocha huyo.
Kwa upande wa nyota wa Vipers, Siraj Setam, alisema: “Tumekuja kwa ajili ya kuchukua pointi tatu, hilo lipo wazi. Tulicheza na Yanga wakati fulani na sasa tumerejea kwa ajili ya Simba.”