Klabu ya Yanga imepangwa kucheza na Klabu ya Rivers United ya Nigeria kwenye hatua ya Robo Fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Katika droo hiyo iliyochezeshwa usiku huu wa Aprili 5, 2023 jijini Cairo nchini Misri, Yanga wataanzia ugenini na kumalizia nyumbani katika Dimba la Mkapa.
Ikumbukwe kuwa, mechi hii itakuwa ni kisasi kwa Yanga ambao wana kumbukumbu ya kuondolewa na Rivers United kwenye michuano ya Kombe la Mabingwa Afrika katika hatua ya awali msimu wa mwaka 2021/22 baada kufungwa bao 1-0 nyumbani kisha wakaenda kufungwa bao 1-0 nchini Nigeria.
Mechi nyingine za robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ni kati ya; USM Alger (Algeria) vs AS FAR Rabat (Morocco) US Monastirienne (Tunisia) vs ASEC Mimosas (Ivory Coast) Pyramids FC (Misri) vs Marumo Gallants (Afrika Kusini).
Mechi za mzunguko wa kwanza zitapigwa kati ya Aprili 21-23, 2023 wakati mechi za marudiano (mkondo wa pili) zikipigwa kati ya Aprili 28 -30, 2023.
Aidha, mshindi kati ya Yanga na Rivers United atakutana na mshindi kati ya Pyramis na Marumo Gallants kwenye hatua ya Nusu Fainali wakati mshindi kati ya USM Alger na FAR Rabat atakutana na mshindi kati ya US Monastirienne na ASEC Mimosas kwenye nusu fainali.
Mapema hivi karibuni, Nabi alipoulizwa kuwa angependa Yanga ipangiwe na timu gani, aliitaja River United huku akiweka wazi kuwa anataka kulipa kisasi cha kufungwa msimu uliopita ambapo walitolewa kwenye hatua ya awali.