Home Habari za michezo WAPINZANI WA YANGA CAF KUTUA BONGO LEO….KOCHA WAO AITAJA SIMBA MWANZO MWISHO..

WAPINZANI WA YANGA CAF KUTUA BONGO LEO….KOCHA WAO AITAJA SIMBA MWANZO MWISHO..

Maruno Gallants

Wapinzani wa Young Africans katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Marumo Gallants wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam leo Jumatatu (Mei 08) tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali.

Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo huo keshokutwa Jumatano (Mei 10) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam saa kumi jioni, kisha itakwenda Afrika Kusini Mei 17, kwa ajili ya Mchezo wa Mkondo wa Pili.

Habari kutoka Afrika Kusini zinaeleza kuwa Marumo wameanza safari ya kuelekea Dar es salaam, baada ya kumaliza mchezo wao wa Ligi Kuu ya dhidi ya Mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita.

“Marumo Jumatatu (leo) wanatarajiwa kuwa huko Dar, wanatarajiwa kutua hiyo siku tayari kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Young Africans, kama ambavyo unafahamu mchezo ni Jumatano hivyo watakuwa na siku mbili za kujiandaa ambazo ni Jumatatu yenyewe na Jumanne.”

“Pengine Marumo wangewahi kuja Tanzania mapema lakini kumbuka Jumapili walikuwa na mchezo mgumu wa ligi kuu dhidi ya Mamelodi hivyo utaona ni kwa jinsi gani ratiba zao ziliwabana.” Imeeleza taarifa kutoka Afrika Kusini

Marumo Gallant ilifanikiwa kufika Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya Pyramid ya Misri, huku Young Africans ikiibamiza Rivers United ya Nigeria kwa ushindi wa jumla wa 2-0.

Marumo Gallants juzi Mei 6 wametoka kupoteza mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Mamelod Sundowns kwa kuchezea kichapo cha mabao 2-0.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili kusaka ushindi ili kutinga hatua ya fainali.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Marumo Gallants , Dylan Kerr amesema anakuja Tanzania kupambana na Young Africans huku akifahamu ubora wa mashabiki walionao ikiwa ni miongoni mwa silaha za timu za Tanzania.

Marumo wanatarajia kuvaana na Young Africans kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika itakayopigwa Mei 10, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kerr aliyewahi kuinoa Simba SC msimu wa 2015-16 amesema si mechi rahisi kwao kulingana na ratiba ngumu waliyonayo hivi karibuni hasa kwenye Ligi Kuu Afrika Kusini ambapo wanapambana kusalia kwenye ligi hiyo.

“Binafsi niseme nimeguswa na kuja kwangu tena Tanzania kutokana na ushirika wangu na Simba SC nilipokuja kuifundisha wakati huo na ni muda mzuri pia kurejea Tanzania kwa sasa.”

“Tutakuja kupambana, kufanya kile tulichokifanya kwenye mechi tisa tulizocheza ndani ya siku 28, ni ratiba ngumu tuliyoipitia hasa kwenye ligi lakini nilipofika hapa (Marumo) mara ya kwanza tulionesha kupambana na mpaka hapa tulipofika wachezaji wamefanya kazi kubwa, naamini tutaendelea kupambana,” amesema Kerr.

Kocha huyo raia wa Uingeeza amesema anafahamu upinzani wa mashabiki uwanjani atakaokutana nao kutokana na ubora wa ushangiliaji wa mashabiki wa timu za Tanzania akifafanua wamekuwa na utofauti na wa timu nyingine Afrika.

Niseme mashabiki wa Afrika wamekuwa tofauti kila kanda, Kaskazini wana aina yao kali ya ushangiliaji, sitaki kuwakosea heshima wengine lakini mashabiki wa Simba SC na Young Africans wamekuwa na ushangiliaji mzuri na wa kuvutia mno dhidi ya wapinzani,” amesema Kerr.

Pia aliongeza kuwa timu za Tanzania zinaelekea kwenye mafanikio makubwa Afrika kutokana na uwekezaji uliopo kwenye sekta hiyo akilinganisha na wakati ambao anaiona Simba SC, akikiri kwa sasa hali ni tofauti.

Marumo inatarajia kurudiana na Young Africans Mei 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng Rustenburg, mchezo unaotarajia kupigwa kuanzia saa 1.00 usiku.

SOMA NA HII  WAKATI MO DEWJI AKITIA MZIGO SIMBA, BILIONE YANGA AJIBU MAPIGO