MABINGWA wa Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC, Yanga wanaweza kukumbana na rungu la kufungiwa kusajili katika madirisha matatu ya usajili ikiwa ni pamoja na kuondolewa msimu ujao kwenye michuano ya Kimataifa.
Uamuzi huo unaweza kufanywa muda wowote, kutokana na Yanga kushindwa kulipa kwa wakati deni la aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Luc Eymael.
Eymael aliiburuza Yanga kwa Shirikisho la Kimataifa la Soka Duniani (FIFA) kwa kosa la kuchelewa kumlipa madai yake miezi michache baada ya kibarua chake kuota nyasi, Septemba 2021.Hata hivyo miamba hiyo ya soka la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki ilikubali kumlipa kocha huyo kwa awamu.
Kwa mujibu wa notisi ya malipo ya Eymael, Yanga ilipaswa kumalizana naye ndani ya siku 45 huku kuanzia Juni 9 mwaka huu wakitakiwa kulipa na riba ya asilimia tano hadi juzi Ijumaa ambapo ilikuwa siku ya mwisho kumaliza deni la Dola 66,000 ambazo ni zaidi ya Sh. 157milioni.
Kocha huyo, amesemai kuwa asilaumiwe kwa kile ambacho FIFA inaweza kufanya kufuatia Yanga kushindwa kukamilisha kile ambacho walikubaliana kuhusu malipo yake kwani hadi siku ya mwisho, juzi walikuwa wamemlipa nusu ya kiwango ambacho alitakiwa kupata.
“Nimekuwa nikifanya nao mawasiliano lakini naona wamekuwa kimya, kwa kuwa hili suala limefika kwenye mamlaka husika kwa hiyo tutaona kile ambacho wataamua, wanaweza pia kuingia kwenye adhabu ya kupokonywa pointi tisa,”
“Mwaka 2018 au 2017, Amazulu walikuwa na kesi kama hii, hawakulipa hivyo FIFA iliwalazimisha kulipa au kushuka daraja kabla ya msimu mpya kuanza, siku zote hakuna aliye juu ya sheria,” alisema kocha huyo.
Kwa mujibu wa Eymael inamaana kuwa hadi siku ya mwisho ya malipo yote kufanywa, Yanga ilikuwa imemlipa Dola 33,000 (Sh78.8 milioni).
Yanga inaweza kuwa kwenye wakati mgumu zaidi kama FIFA itachukua maamuzi hayo kutokana na baadhi ya wachezaji wao muhimu kuwa mbioni kutimka akiwemo Fiston Mayele anayehusishwa na klabu mbalimbali kubwa ndani na nje ya Afrika kufuatia kuwa mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alitafutwa jana ili kutoa ufafanuzi wa jambo hilo, lakini simu yake haikupokelewa sawa na ilivyokuwa kwa Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo.