Home Habari za michezo KUHUSU DILI GOLIKIPA MBRAZILI KUTUA SIMBA…UKWELI WOTE HUU HAPA…

KUHUSU DILI GOLIKIPA MBRAZILI KUTUA SIMBA…UKWELI WOTE HUU HAPA…

Tetesi za Usajili Simba

SIMBA imeendelea kutoa ‘Thank You’ kwa baadhi ya mastaa wake, lakini huku ikiendelea kusajili nyota wapya na kwa taarifa yako tu ni kwamba msimu ujao langoni mwa timu hiyo atasimama chuma cha Kibrazili baada ya kuanza mazungumzo na Caique Luiz Santos da Purificacao wa Ypiranga FC.

Kama mipango itaenda sawa basi kipa huyo ndiye atakayechukua nafasi ya Beno Kakolanya aliyetemwa na kudaiwa ametua Singida Big Stars na atakayeziba kwa muda nafasi ya Aishi Manula anayejiuguza kwa sasa na atakayekuwa nje ya muda mrefu hadi Novemba.

Awali  Simba ilikuwa  inatafuta kipa mpya wa kigeni baada ya Aishi Manula kupata jeraha la nyonga litakalomuweka nje, huku Beno naye akitimka na kulikuwa na majina mezani yakiwamo ya Fabien Mutombora na Alfred Macumu kutoka Vipers, huku jina lingine likifichwa.

Majina hayo ni mapendekezo ya Kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kutoka Brazili, lakini Mwanaspoti limefukunyua hadi kulipa jina lililofichwa kuwa ni la Caique.

Caique mwenye umri wa miaka 25, akiwa amezaliwa Julai 31, 1997 katika mji wa Salvador huko Brazili kwa sasa anaichezea Ypiranga RS inayoshiriki Ligi ya Campeonato Brasileiro Serie C, sawa na First League hapa Tanzania akiwa kipa namba moja.

Kipa huyo mwenye urefu wa futi 6 na inchi 5 alikulia kwenye akademi ya ES Victoria mwaka 2016, kabla ya kuitema na kwenda CSA ya Brazil sambamba na Ermis Aradippou ya Cyprus na Rochester NY ya Marekani kwa nyakati na misimu tofauti.

Caique alikuwa kipa namba moja wa kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 (Brazil U-20), mwaka 2016 na 2017 kikishiriki michuano mbali mbali ya kimataifa kuonyesha kwamba ni mzoefu wa kutosha, kitu ambacho Simba kwa sasa inahitaji kipa wa aina hiyo.

Wakati akiwa kwenye kikosi hicho cha timu ya taifa alikuwa na nyota wengine wanaowika kwa sasa kwenye soka duniani wakiwemo Richarlison de Andrade wa Tottenham, Douglas Luiz wa Aston Villa, Lucas Paqueta wa West Ham na Gabriel Magalhes wa Arsenal.

Utamu zaidi ni kwamba uwezo wa Caique wa kutumia miguu yote kwenye kupiga mipira, pia nje ya kudaka michomo inambeba kwani linaonekana ni kama jibu kwa Yanga ambayo inajivunia Djigui Diarra anayesifika kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi na kuchezesha timu uwanjani.

Chanzo makini kutoka Simba (jina tunalo) kimesema kuwa tayari klabu hiyo imemtumia mkataba Caique aliyeko Brazil na akiridhia na kusaini basi ataambatana na kocha Robertinho aliye mapumzikoni nchini humo kuja naye Tanzania kujiunga kwa ajili ya kwenda kambini ya maandalizi ya msimu itakayopkuwepo Uturuki.

Sambamba na kipa huyo Simba imeendelea na usajili wa wachezaji wa maeneo mengine na hadi sasa  tayari imemsainisha mkataba wa miaka miwili winga Mcameroon Leandre Onana aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Rwanda akiifungia timu yake ya Rayon Sports mabao 17.

SOMA NA HII  KIMENUKA SIMBA...DEWJI ATANGAZA KUMTAMBUA MGUNDA KAMA KOCHA MKUU WA TIMU...