MABOSI wa Simba, wameweka wazi mkakati wao ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika michuano ya Afrika Super League, bila ya kuangalia watapangwa na mpinzani wa aina gani wakiwemo Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.
Simba wametoa kauli hiyo kufuatia kupokea maofisa wa Shirikisho la Soka Afrika ‘CAF’ ambao wapo nchini kwa ajili ya ukaguzi wa maandalizi ya michuano hiyo inayotarajia kuanza Oktoba mwaka huu, ambapo ufunguzi wake utafanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa timu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Gain’ alisema kuwa, mikakati yao mikubwa ni kuhakikisha wanafanya vizuri bila ya kuangalia watakutana na wapinzani wa aina gani katika michuano hiyo.
“Maandalizi ya Afrika Super League kwa upande wa Simba yameshaanza kwa sababu tumeendelea kupokea wageni mbalimbali ambao ni maofisa wa CAF, kwa ajili ya ukaguzi na maandalizi ya ufunguzi wa mashindano yenyewe ambayo yatazinduliwa hapa nchini.
“Binafsi kwetu hili ni jambo kubwa kwa kupata nafasi ya kushiriki katika michuano hii mikubwa, malengo yetu ni kuona tunafika mbali kwa timu kuweza kupata matokeo mazuri katika kila mchezo bila ya kujali tunakutana na mpinzani wa aina gani kwa sababu uzoefu wetu ni mkubwa katika soka la Afrika,” alisema Try Again.