Baada ya kukitazama kikosi cha Simba katika michezo mitatu iliyopita, nyota wa zamani wa Yanga, Pan na Timu ya Taifa, Rashid Idd ‘Chama’ amesema timu hiyo bado haijapata muunganiko na mashabiki wanapaswa kuipa muda.
Tangu iliporejea kutoka Uturuki ilikoweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya, Simba imecheza michezo mitatu na kufunga mabao mawili ndani ya dakika 270 huku baadhi ya nyota wake wapya wakishindwa kuonyesha makali.
Simba iliichapa Power Dynamos ya Zambia mabao 2-0, kwenye Simba Day Agosti 6, mwaka huu, kisha ikatoka sare na Singida Fountain Gate FC kwenye Ngao ya Jamii na kumaliza kwa suluhu dhidi ya Yanga kwenye fainali kabla ya kushinda kwa penalti 3-1.
Chama aliyekuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, kilichocheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 1980 kule Nigeria, alisema Simba imeshusha majembe kwenye dirisha la usajili kilichobaki ni kutengeneza muunganiko ili timu itishe kwenye michuano iliyo mbele yake msimu huu.
Chama aliyeipandisha Mashujaa Ligi Kuu alisema baadhi ya wachezaji wameshindwa kutumika kwenye kikosi hicho licha ya kuwa na ubora, wanapaswa kuichukulia hiyo kama changamoto na kurudi mazoezini na kujipanga upya ili walishawishi benchi la ufundi.
“Simba imesajili wachezaji wazuri lakini inatakiwa wawape muda maana wanahitaji kujenga muunganiko.
“Phiri (Moses) ni mchezaji mzuri lakini anakosa nafasi ya kucheza kwa hiyo anatakiwa akubali changamoto iliyomkuta apambanie namba,” alisema Chama
Shabiki wa Simba jijini hapa, Mwashumu Magesa alisema hawana wasiwasi na kikosi chao baada ya kutwaa ngao safari ya kutetea mataji waliyoyapoteza kwa watani wao Yanga misimu miwili ndiyo imeanza huku akitamba mastaa waliowasajili watawapa heshima kubwa.