MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga, amesema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwatambua wapinzani wao katika hatua ya makundi, watacheza kwa kutafuta ushindi na kuwafurahisha mashabiki.
Juzi Ijumaa, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilichezesha droo na kupanga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga imeangukia Kundi D ikiwa na timu za Al Ahly ambao ni mabingwa watetezi wakitokea Misri, CR Belouizdad (Algeria), Medeama (Ghana). Kundi hilo lina Waarabu wawili, Al Ahly na CR Belouizdad.
Hii ni historia nyingine Yanga inakwenda kuandika baada ya kuyeyusha miaka 25 bila kushiriki hatua ya makundi kwenye mashindano hayo.
Kocha huyo amesema: “Tunatambua wapinzani wetu katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni imara, nasi tutafanya kazi kutafuta ushindi. Ni kazi kubwa kwenye mechi za kimataifa hilo tunalitambua lakini tutacheza kwa umakini kupata ushindi na kuwafurahisha.
“Wachezaji wapo tayari kuona tunapata ushindi na makosa kwenye mechi zilizopita tunafanyia kazi ili kuwa bora na imara zaidi.
“Mashabiki wakijitokeza kwa wingi uwanjani inatuongezea nguvu ya kupata matokeo. Imani yetu ni kuona tunakuwa na mwendo mzuri kwenye mechi ambazo tunacheza.”