Home Habari za michezo MAGORI:- MECHI YA KESHO NA AL AHLY…SIMBA TUSIDANGANYANE….

MAGORI:- MECHI YA KESHO NA AL AHLY…SIMBA TUSIDANGANYANE….

Habari za Simba

Crescentius Magori ambaye ni Mshauri wa Rais wa heshima wa Simba Bw.Mohammed Dewji, amesema kuelekea mechi yao ya marudiano hapo kesho dhidi ya Al Ahly huko Misri basi wachezaji wao inabidi wajitoe ili kuupata ushindi maana hiyo ni timu ngumu sana ikiwa kwao.

“Simba tuna wakati mgumu sana katika mchezo na Al Ahly wa marudio na wala tusidanganyane,inabidi wachezaji wakafanye kazi zaidi na kujitolea,ingawa hakuna kinachoshindikana kwani mwaka 2003 tuliwatoa mabingwa Zamaleki enzi hizo huko huko kwao kipindi ambacho wengi hapa Tanzania walikua wametukatia tamaa” amesema Magori.

Aidha katika hatua nyingine, MKURUGENZI wa Maendeleo ya Soka Duniani wa Fifa, Arsene Wenger ambaye ni kocha wa zamani wa Arsenal, amewapongeza wachezaji wa Simba kwa kiwango bora katika dakika 45 za kipindi cha pili kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuano ya African Football League dhidi ya Al Ahly.

Simba ilionyesha kiwango cha juu katika kipindi cha pili cha mchezo huo kwenye Uwanja wa Mkapa juzi uliohudhuriwa na watu maarufu akiwemo rais wa Fifa, Gianni Infantino.

Akiwa sambamba na Infantino, rais wa CAF, Patrice Motsepe pamoja na rais wa TFF, Wallace Karia, kocha huyo mzoefu duniani alikitembelea kikosi cha Simba katika chumba cha wachezaji uwanjani hapo na kuwaambia mastaa kuwa kama wangecheza kipindi cha kwanza kama walivyofanya kile cha pili walikuwa na uwezo wa kuibuka na ushindi.

Kwa lugha ya Kiingereza, Wenger hakuwa na maneno mengi zaidi ya kuwapongeza wachezaji wa Simba kwa kiwango walichokionyesha kipindi cha pili ambapo walisawazisha bao kupitia kwa Kibu Denis na kufunga la kuongoza kupitia kwa Sadio Kanoute kabla ya Al Ahly kuchomoa.

“Wenger alitueleza kuwa kipindi cha kwanza tulicheza chini ya kiwango hatukufuata vizuri maelekezo ya mwalimu, lakini akatupongeza kwa jinsi tulivyocheza kipindi cha pili. Alisema kama tungecheza vile vipindi vyote tulikuwa na nafasi ya kupata ushindi kwenye mechi hii.

“Hakuongea maneno mengi, lakini kila alipokuwa anazungumza wale walioongozana naye walikuwa wakitikisa vichwa kuonyesha kukubaliana naye,” alisema staa mmoja wa kikosi cha kwanza cha Simba.

Nyota huyo alisema baada ya hapo walipata nafasi ya kupiga naye picha na akaondoka akaenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya Al Ahly.

Kwa upande wake, rais wa heshima wa Simba, Mohammed Dewji naye aliwatembelea wachezaji na kuwapa moyo wa kufanya vizuri ugenini ili kuiheshimisha Simba na nchi.

“Mo alikuja na kutueleza kuwa tuende tukapambane ugenini na kila kitu kinawezekana,” alisema mchezaji huyo.

Simba ilitarajiwa kuondoka jana kwenda Misri kwa ajili ya mchezo utakaopigwa keshokutwa dhidi ya Al Ahly ambapo mshindi atakutana na Petro de Luanda ya Angola au Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

SOMA NA HII  MANARA:- YANGA TUNACHEZA STAILI YA 'PPP'.....'APOROMOSHA MVUA YA MANENO' KWA NABI....