Home Habari za michezo WAFAHAMU NNJE NDANI WAPINZAI WA SIMBA NA YANGA LIGI YA MABINGWA AFRIKA….

WAFAHAMU NNJE NDANI WAPINZAI WA SIMBA NA YANGA LIGI YA MABINGWA AFRIKA….

Habari za Michezo

Makocha wa Simba na Yanga walisema mapema, wapo tayari kupangwa na timu yoyote katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mashabiki na wapenzi wa klabu hizo nazo wakatambiana sana mtaani kwamba timu zao zipo tayari kukabili mpinzani yeyote ili kuonyesha ukubwa wao.

Sasa jana jioni, droo ya mechi za makundi ikafanyika jijini Johannesburg, Afrika Kusini na timu hizo zikajikuta zikiangukia kwenye makundi tofauti sambamba na vigogo vya soka barani Afrika na sasa ni nafasi yao kuthibitisha ukubwa wao kwenye soka kwenye michuano hiyo ili kusaka tiketi za kucheza robo fainali.

Yanga inayoshiriki makundi baada ya kupita miaka 25 imepangwa Kundi D pamoja na watetezi, Al Ahly ya Misri, CR Belouizdad ya Algeria na Medeama ya Ghana, wakati Simba ikiwekwa Kundi B na Wydad CA ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Timu hizo zimekutanishwa na timu tano tofauti ambazo zimeshawahi kucheza nazo na kupoteza mechi katika michuano tofauti kwa ngazi za klabu barani Afrika.

Simba inakutana tena na Wydad Casablanca iliyowatoa katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya 1-1, pia ikipewa Asec Mimosas iliyowachapa mabao 3-0 katika mechi ya mwisho baina yao kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021/2022, japo awali Simba ilishinda nyumbani kwa mabao 3-1.

Kundini humo pia inakutana na Jwaneng Galaxy iliyoing’oa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2021/2022 kwa faida ya bao la ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya mabao 3-3, Simba ilishinda ugenini 2-0 na kulala nyumbani mabao 3-1.

Kwa upande wa Yanga, ina kisasi dhidi ya Al Ahly iliyowatoa mara nne tofauti katika michuano ya klabu Afrika na katika mechi nane walizokutana, Yanga imeshinda moja tu, ikitoka sare mbili na mabingwa hao wa kihistoria wa michuano hiyo ikitwaa taji mara 11, wakishinda mechi tano.

Wapinzani wa Simba

Wydad, Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy zilizo kundi B pamoja na Simba zimekuwa na sifa na historia tofauti katika michuano ya klabu Afrika kama zinavyoainishwa na gazeti hili.

Kwa mujibu wa mtandao wa www.trasfermarkt.com, thamani ya kikosi cha Wydad ni Euro 19.05 milioni na mchezaji ghali zaidi ni Yahya Jebrane ambaye ana thamani ya Euro 1.8 milioni.

Timu hiyo ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Morocco mara 22 ikiwa na miaka 86 tangu ilipoanzishwa 1937 inanolewa na kocha raia wa Morocco, Adil Ramzi na inatumia Uwanja wa Mohammed wa V unaoingiza mashabiki 45,000.

Bouly Sambou ndiye mchezaji tegemeo zaidi kwa Wydad kutokana na uwezo wake wa kufumania nyavu ambapo kwenye mashindano hayo msimu huu amefunga bao moja.

Kiungo mkabaji, Yahya Jebrane ambaye ndiye nahodha wa Wydad ni mchezaji mwingine anayepaswa kuchungwa zaidi na Simba kwani ndiye mjenzi wa mashambulizi ya timu hiyo ya Morocco, ana uwezo mkubwa wa kuilinda safu ya ulinzi lakini pia amekuwa akishiriki katika kufunga mabao na kupiga pasi za mwisho.

Wamekuwa wakitumia jezi zenye rangi nyekundu na nyeupe lakini pia hutumia zile za rangi ya bluu kama jezi namba tatu.

Asec Mimosas

Ni kati ya timu zilizoweka alama ya kuwahi kutwaa ubingwa wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakifanya hivyo mwaka 1998 lakini pia kwa nyakati tofauti wamewahi kuingia fainali, nusu fainali na robo fainali.

Timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1948 imekuwa ikitumia jezi za njano zenye michirizi ya rangi nyeusi zikiwa nyumbani na ugenini huwa inapendelea kutimia jezi za rangi nyeusi.

Katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu imekuwa ikitumia Uwanja wa De la Paix uliopo Bouake, Ivory Coast unaoingiza idadi ya mashabiki wasiopungua 35,000 na inanolewa na kocha Julien Chevalier ambaye ni raia wa Ufaransa.

Jwaneng Galaxy

Mafanikio makubwa ya Jwaneng Galaxy kwenye mashindano ya Klabu Afrika ni kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2021/2022 ambapo walishika mkia dhidi ya timu za Belouizdad, Esperance na Etoile du Sahel,

Wanatumia jezi za rangi nyeupe zenye ufito mwekundu wakiwa nyumbani katika Uwanja wao wa Taifa wa Botswana unaoingiza mashabiki wapatao 25,000.

Kocha raia wa Afrika Kusini, Morena Ramorebolli ndiye anaionoa timu hiyo na waliingia hatua ya makundi kwa kuitoa Orlando Pirates kwa penalti 6-5 baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Wapinzani wa Yanga

Bila ya shaka Al Ahly ndio timu tishio zaidi kwa Kundi D kutokana na mafanikio makubwa, uzoefu na ubora ilionao dhidi ya Yanga, Medeama na Belouizdad.

Kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarkt, thamani ya kikosi cha Al Ahly kwa sasa ni Euro 30.35 milioni (Sh80 bilioni) na mchezaji ghali zaidi ni Aliou Dieng mwenye thamani ya Euro 4.5 milioni (Sh11.8 bilioni).

Uwanja wa kimataifa wa Cairo ndio umekuwa ukitumiwa na miamba hiyo ya Misri ambayo inapokuwa nyumbani huvaa jezi za rangi nyekundu na ugenini huvaa za rangi nyeusi.

Kocha wa zamani wa FC Basel, FC Cologne, VfL Bochum na St. Gallen, Marcel Kohler ndiye anainoa timu hiyo ambayo ndio bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Al Ahly ndio mabingwa wa kihistoria wa mashindano hayo wakiwa wametwaa taji hilo mara 11 lakini kiujumla wametwaa mataji 24 ya mashindano ya klabu Afrika.

Ikumbukwe Al Ahly wametinga hatua ya makundi kwa kuitoa St. George ya Ethiopia kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-0.

CR Belouizdad

Ni timu inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Sven Vandenbroeck ikiwa na umri wa miaka 61 kwani imeanzishwa mwaka 1962.

Miamba hiyo ya Algeria imekuwa ikitumia jezi za rangi nyekundu kwa mechi zao za nyumbani, nyeupe pindi inapokuwa ugenini na jezi yao ya tatu ina rangi ya bluu.

Ni kati ya timu zenye mafanikio makubwa zaidi nchini Algeria ikiwa imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo mara nane, Kombe la Chama cha Soka Algeria mara nane, mataji mawili ya Kombe la Ligi Algeria na imetwaa makombe mawili ya mashindano ya Maghreb.

Mafanikio makubwa ya CR Belouizdad katika mashindano ya klabu Afrika ni kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 1996 wakipoteza mbele ya AC Sodigraf ya iliyokuwa Zaire, sasa hivi DR Congo.

Kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com, thamani ya sasa ya kikosi cha CR Belouizdad ni Euro 10.95 milioni na wachezaji wenye thamani kubwa zaidi ni beki Houcine Benayada na winga Zinedine Boutmene ambao kila mmoja ana thamani ya Euro 750,000.

Nyota tishio katika kikosi chao ni mshambuliaji wa Cameroon, Wamba Leonel ambaye ameifungia timu hiyo mabao matatu kati ya sita iliyofunga katika hatua ya awali.

Medeama

Kocha mzawa Ignatius Osei-Fosu ndiye anainoa Medeama ambayo kikosi chake kinaundwa na wachezaji wengi wazawa huku wawili tu wakiwa wa kigeni ambao wanatokea Ivory Coast.

Mafanikio makubwa ya Medeama ni kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016 ambapo walimaliza wakiwa katika nafasi ya tatu.

Imeingia katika hatua ya makundi baada ya kuitupa nje Horoya ya Guinea kwa ushindi wa mabao 4-3.

Inapokuwa nyumbani huvaa jezi zenye rangi ya bluu zenye michirizi ya njano.

Hakuna presha

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kuwa wapo tayari kwa kibarua kilicho mbele yao.

“Hakuna kundi rahisi katika haya mashindano. Hizo timu zote kwenye kundi letu zilishawahi kutufunga na sisi tulishawafunga. Kundi ni gumu hivyo tunahitaji kufanya kazi hasa tuweze kufanya vizuri na kutimiza malengo yetu,” alisema Try Again.

Ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema wapo tayari kupambana na wapinzani wao kwenye kundi walilopo.

“Ukiwa mfuatiliaji wa soka utabaini kwamba kundi A na D ndio makundi magumu. Tupo dhidi ya timu ngumu lakini hii ndio hatua ya kuitambulisha Yanga. Naamini tukishirikiana vyema tutafanya vizuri,” alisema Kamwe.

SOMA NA HII  HATIMAYE MGUNDA APASUKA UKWELI KUHUSU KUWA KOCHA MSAIDIZI SIMBA...AGUSIA ISHU YA KUSEPA...