Home Habari za michezo GSM DAY YAIFANYA YANGA KUANDIKA HISTORIA HII MPYA CAF….MANJI NA UTAJIRI WAKE...

GSM DAY YAIFANYA YANGA KUANDIKA HISTORIA HII MPYA CAF….MANJI NA UTAJIRI WAKE ALISHINDWA…

Habari za Yanga

YANGA imeandika historia baada ya ushindi wa kwanza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ilipoichapa Medeama ya Ghana kwa mabao 3-0.

Ushindi huo uliokoleza rekodi tamu ya Yanga ya Kocha Miguel Gamondi ya kufunga mabao mengi kipindi cha pili ulikuwa ni wa kwanza kwa timu hiyo, kwani ilikuwa haijawahi kushinda kwenye hatua ya makundi katika michuano hiyo iliposhiriki mara ya kwanza mwaka 1998.

Msimu huu ikicheza mara ya pili baada ya kupita miaka 25, Yanga ilianza kwa kufungwa na CR Belouizdad ya Algeria kisha ikatoka sare ya 1-1 mbele ya Al Ahly ya Misri na Medeama, lakini ilipambana na kupata ushindi huo ulioiweka pazuri kwenye Kundi D ikifikisha pointi tano na mabao matano nyuma ya Al Ahly.

Hata hivyo, Al Ahly ina mechi moja mkononi dhidi ya CR Belouizdad na inaongoza kwa kuwa imefunga mabao manne na kufungwa moja tofauti na Yanga iliyofunga matano na kufungwa matano katika mechi zake nne.

Licha ya ushindi huo, bado Yanga itajilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi mnono zaidi kwani ilitengeneza nafasi nyingi ilizozipoteza kwenye kipindi cha kwanza na kile cha pili zilizowafanya mashabiki wa klabu hiyo kuwa wanyonge kwa muda mrefu, huku wageni nao wakionyesha kucheza kichovu kwa muda mrefu.

Pacome, alifunga bao dakika ya 33 baada ya kupokea pasi ya Khalid Aucho kisha kukokota mpira na kuwahadaa mabeki wa Medeama kabla ya kupiga shuti kali lililowapa faraja mashabiki na kuitoa timu kwenye presha kwani ni bao lililodumu hadi mapumziko.

Mabao mengine ya Yanga yalifungwa kipindi cha pili na Bakari Mwamnyeto dakika ya 61 akiusindikiza mpira wa kichwa wa Kennedy Musonda baada ya kona ya Yao Kouassi, kisha Mudathir Yahya kupiga la tatu dakika ya 70 na kuwafanya Yanga kubadili upepo wa historia kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa.

SOMA NA HII  TAKWIMU ZAENDELEA KUMBURUZA KIBU DENIS...FAILI LAKE LOTE SIMBA HILI HAPA