WIKI iliyopita pale Simba alitambulishwa kinda anayeitwa Saleh Masoud Karabaka. Alinunuliwa hapo hapo Zanzibar, akavaa jezi hapo hapo Zanzibar, akafunga bao hapo hapo Zanzibar.
Wapo waliotumia nafasi hiyo kumhukumu kijana Karabaka, lakini ukweli ni kwamba kuna mashabiki wa Simba walioumia kuuona utambulisho wa kwanza wa timu yao katika dirisha la uhamisho. Walitaka mtu au watu zaidi ya Karabaka.
Hata hivyo, kuna waliojifariji hata watani wao wiki mbili zilizopita walikuwa wamemchukua mchezaji kinda kutoka Zanzibar anaiyetwa Shekhan Ibrahim Khamis.
Ngoma ikawa droo kidogo. Kwamba labda timu zote mbili zimesajili wachezaji wa baadae.
Lakini juzi shughuli rasmi imeanza pale Msimbazi. Ametambulishwa kiungo kutoka Senegal, Babacar Sarr. Aliyekuwa staa wa Monastir ya Tunisia. Huyu ndiye aina ya mchezaji ambaye mashabiki wa Simba walikuwa wanamsubiri.
Tumeanza kuona picha zake akikabana na Cristiano Ronaldo. Nadhani ilikuwa katika michuano ya Kombe la Asia. Tumeanza kuona mbwembwe nyingi mitandaoni. Huyu ndiye aina ya mchezaji ambaye mashabiki wa Simba wanaamini alipaswa kuanza kusajiliwa kabla ya Karabaka.
Baada ya hapo Simba inatarajiwa kushusha vifaa vingi kutoka nje. Sidhani kama kuna uhamisho wa wachezaji wa ndani ambao unaweza kuwasisimua mashabiki wa Simba kwa sasa. Viwango vya wachezaji wa ndani vinaonekana kuwa vya kawaida.
Labda wamsajili mchezaji wa ndani kutoka Azam au Yanga, lakini sijaona uhamisho wa mchezaji wa ndani kutoka katika klabu nyingine ambazo sio Azam na Yanga ambao utawasisimua mashabiki. Ni kwa sababu wamesajiliwa wachezaji wengi wa aina hiyo katika miaka ya karibuni lakini wameshindwa kumudu muziki.
Sarr ndiye usajili uliokuwa unasubiriwa na sisi tumebaki kujiuliza kama usajili wake ni mwanzo wa zama mpya za Simba kuleta wachezaji ambao moja kwa moja watakuja kuingia katika kikosi cha kwanza na kufanya mambo makubwa pamoja na kupunguza umuhimu wa wachezaji kama kina Clatous Chama uwanjani.
Wasifu wake ni mkubwa, lakini Simba imekuwa na bahati mbaya katika miaka ya karibuni katika wachezaji ambao imekuwa ikiwanasa.
Haishangazi kuona katika miaka ya karibuni wachezaji waliongia moja kwa moja katika kikosi Fondoh Che Malone na Fabrice Ngoma.
Wengine inawezekana hawakuwa bora sana, au walikumbana na majeraha, au walikuwa na matatizo ya utovu wa nidhamu. Hii ilisababisha timu iendelee kuwa katika mikono ya wachezaji wale wale wa zamani.
Kuna wakati unaweza kuwabebesha zigo la lawama viongozi kuna wakati hauwezi kuwabebesha zigo la lawama. Jaribu kufikiria kwamba mchezaji kama Jose Luis Miquissone aliporudishwa kikosini bado ameonekana kusuasua licha ya kuondoka akiwa wa moto.
Kule kwa wenzao wamekuwa na bahati ya kupatia sana na kukosea kidogo. Mfano ni namna ambavyo wachezaji wao wamekuwa wakiingia moja kwa moja kikosi na kung’ara wenyewe takribani kila msimu huku timu yao ikiendelea kuimarika.
Upande wa kulia wa Yanga baada ya kuondoka kwa Juma Abdul wamekuwepo Shomari Kibwana, Djuma Shaban na Yao Kouassi. Wote hawa wamecheza katika kikosi cha kwanza kwa umahiri mkubwa. Walikuwepo kina Mukoko lakini wameondoka na timu ikaendelea kuwa imara kwa Yannick Bangala na Khalid Aucho. Leo pia wana Mudathir Yahya.
Tazama namna ambavyo msimu uliopita Yanga waliondokewa na Fei Toto, Fiston Mayele, Djuma pamoja na Bangala lakini wamerudi msimu huu wakiwa moto kwa sababu wameendelea kusajili wachezaji wazuri kikosini pamoja na kuamsha wachezaji wa ndani kina Nickson Kibabage.
Simba wanahitaji aina hii ya mabadiliko katika kikosi na kupata bahati ya kuwa na wachezaji ambao wanakuja katika kikosi na kushindana. Wanakuja katika kikosi na kupunguza umuhimu wa baadhi ya wachezaji wanaojiona mastaa na ambao wanasumbua timu.
Sasa tunamsubiri Babacar Sarr. Ni wazi kama akileta makali yake basi moja kwa moja ataleta upinzani kwa akina Sadio Kanoute na Fabrice Ngoma. Lakini zaidi ni katika dunia ya kisasa unahitaji wachezaji ambao wakitokea nje au wakianza wanakuwa na umuhimu ule ule kikosini.
Pale kwa watani wao akitoka Mudathir akaingia Sure Boy unajua aliyeingia uwanjani naye ni mchezaji wa maana. Dunia ya kuwa na kikosi bora cha kwanza imepitwa na wakati. Unahitaji wachezaji wengi bora katika kila nafasi kwa ajili ya kuiweka timu hai kwa dakika zote tisini.
Leo anaanza Ngoma kesho anaanza Sarr na timu inakuwa na mwendo ule ule. Katika hili Simba machaguo yamepungua tangu wakati ule walipokuwa na Chama, Larry Bwalya, Hassan Dilunga, Miquissone, Bernard Morrison, Meddie Kagere, John Bocco na Chris Mugalu ndani ya kikosi kimoja.
Kila la kheri kwa Sarr lakini wakati utaamua kama Simba wameanza vyema kukijenga upya kikosi chao au vinginevyo.
Wakati mwingine sio suala la Simba bali mchezaji mwenyewe kushindwa kumudu mazingira au aina ya soka letu.
Simba haiitaji tena wachezaji wa aina ya Ismail Sawadogo. Inahitaji watu wa maana.
Credit-MwanaSpoti/Edo Kumwembe