Home Habari za michezo BAADA YA KUMALIZA USAJILI….MAAMUZI YA BENCHIKHA KWA MASTAA WAPYA SIMBA HAYA HAPA…

BAADA YA KUMALIZA USAJILI….MAAMUZI YA BENCHIKHA KWA MASTAA WAPYA SIMBA HAYA HAPA…

Habari za Simba leo

SIMBA imewapa mapumziko ya siku 10 mastaa wa timu hiyo baada ya kutoka kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 iliyofika fainali na kufungwa bao 1-0 na Mlandege, lakini kocha mkuu, Abdelhak Benchikha ni kama amewatega kiaina wachezaji wapya waliosajiliwa kupitia dirisha dogo.

Mastaa wapya waliosajiliwa na Simba ni viungo washambuliaji Saleh Karabaka kutoka JKU na Ladack Chasambi (Mtibwa Sugar), kiungo wa mkabaji Msenegali Babacar Sarr na mastraika wawili Mgambia Pa Omar Jobe na Muivory Coast Freddy Michael Kouablan aliyeongoza kwa ufungaji huko Zambia akifunga mabao 14 na asisti nne katika mechi 16 za Ligi Kuu nchini humo.

Kocha Benchikha alisema timu hiyo ilihitaji ongezeko na mabadiliko ya wachezaji kwenye dirisha dogo lililopita, hivyo mastaa waliosajiliwa wanahitaji kuziba moja kwa moja mapengo yaliyokuwepo na kuhakikisha timu inafanya vizuri.

“Tulihitaji mabadiliko na kuongeza watu, waliosajiliwa sasa ni jukumu lao kuonyesha umuhimu wao ndani ya timu. Tunataka kufanya vizuri katika kila michuano tunayoshiriki hivyo kila mchezaji anahitajika kuonyesha kwanini yupo Simba,” alisema Benchikha.

“Tunaendelea kujenga timu itakayokuwa na ushindani na kucheza soka la kuvutia, tutakaporejea naamini tutatengeneza kikosi imara zaidi.”

Beki na kocha zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema wachezaji wapya wamebeba matumaini makubwa hivyo hawapaswi kuwaangusha.

“Mchezaji anaposajiliwa anakuwa anategemewa kufanya makubwa zaidi, hivyo ndivyo ilivyo na kwa hao wa Simba hivyo wakipata nafasi wanatakiwa kuhakikisha wanaonyesha ubora na faida kikosini. Binafsi siwezi kutoa maoni ya moja kwa moja bali nawapa muda niwaone kwanza,” alisema.Simba inatarajia kuingia kambini Jumatano, wiki ijayo kwa ajili ya maandalizi ya mechi zijazo za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazoendelea mwezi ujao.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI SPOTI XTRA JUMANNE