Home Habari za michezo SIMBA MPYA KUJA KIVINGINE KABISA….ONANA AANZA KUJITETEA MAPEMA…..

SIMBA MPYA KUJA KIVINGINE KABISA….ONANA AANZA KUJITETEA MAPEMA…..

Habari za Simba leo

KIPYENGA kimelia Msimbazi na mastaa wote wa Simba ambao hawako kwenye michuano ya Afcon, wanatakiwa kufika kesho Jumatano kambini kwa ajili ya kuanza mazoezi ya kujiandaa na mechi zijazo, huku wenyewe wakitamba kwa kusema “Raundi hii tutaelewana.”

Hiyo ni baada ya kumalizika kwa siku 10 za mapumziko mafupi ambayo benchi la ufundi chini ya kocha mkuu Mualgeria, Abdelhak Benchikha lilitoa kwa mastaa hao ili kupoza miili kutokana na mashindano mbalimbali kusimama kupisha fainali za Afcon.

Hata hivyo, Simba haikutaka wachezaji wake wakae kizembe kwenye mapumziko hayo ndipo ikaamua kumpa kila mchezaji programu maalumu ya mazoezi atakayokuwa anafanya akiwa nyumbani kwake na pale atakaporejea kambini atakaguliwa kama aliitumia kwa ufasaha.

Staa wa Simba Willy Esomba Onana, anayetokea nchini Cameroon amesema mapumziko waliyoyapata yamewasaidia kujitafakari na kujua nini wanatakiwa kufanya watakaporejea uwanjani.

“Tumetumia muda huu kujitafakari wapi tulikosea, wapi tunatakiwa kuongeza nguvu pia kuweka mipango mipya, muda si mrefu tutarudi uwanjani,” alisema Onana ambaye gari lake limewaka tangu kocha Benchikha ameichukua timu.

Kocha wa makipa wa Simba, Dani Cadena amesema watarejea wakiwa imara zaidi na kufanya makubwa.

“Raundi hii tutaelewana, kuna wachezaji wameongezwa na waliokuwepo wamepata muda wa kupumzika, nadhani tukirejea kwa pamoja tutakuwa na nguvu kubwa na mashabiki wataifurahia timu yao,” amesema Cadena mwenye leseni ya ukocha ya UEFA pro.

KUPISHANA AIRPORT

Moja ya vitu ambavyo vinawapa kiburi mashabiki wa Simba ni namna ambavyo chama lao limesheheni mafundi na wataalamu kutoka nje ya nchi ambao kuanzia jana kwa nyakati tofauti walianza kupishana kwenye viwanja vya ndege wakirejea Msimbazi.

Simba ina wachezaji 13 wa kigeni ambapo ukiwatoa Henock Inonga (DR Congo), na Clatous Chama (Zambia), walio katika fainali za Afcon, wengine wote walirejea makwao na sasa ni muda wa kurudi nchini tayari kuitumikia klabu hiyo.

Ayoub Lakred (Morocco), Che Malone Fondoh na Onana (Cameroon), Fabrice Ngoma (DR Congo), Sadio Kanoute (Mali), Saidi Ntibanzokiza (Burundi) na Aubin Kramo (Ivory Coast) na wageni, Babacar Sarr anayetokea Senegal, Freddy Michael Kouablan kutoka Ivory Coast na Mgambia Pa Omar Jobe wote wanatakiwa kuwa kambini na mazoezi rasmi yataanza Alhamisi.

BENCHIKA ALISEMAJE?

Kabla ya kutoa mapumziko hayo, kocha Benchikha aliwasisitiza wachezaji kila mmoja kufanya tafakuri binafsi na kutumia muda huo kupumzika na kufanya mazoezi kiasi huku akijipanga kwa mapinduzi yatakayofanyikia pindi watakaporejea.

“Wakati tunaahirisha kambi kocha alisisitiza tukapumzike huku tukijitafakari, aliongea hilo kwa ukali na kusisitiza kuna mapinduzi na mabadiliko makubwa atayafanya tutakaporejea hivyo tujiandae kukabiliana nayo,” amesema mchezaji wa Simba (jina tunalo).

Simba itatupa karata yake ya kwanza kwenye mechi ya Ligi Kuu Februari 17 mwaka huu dhidi ya Dodoma Jiji, kwenye Uwanja wa Jamuhuri.

SOMA NA HII  MDHAMINI WA SIMBA FREDY 'VUNJA BEI' 'ATUA POLISI'...AITAJA YANGA...