Home Habari za michezo SIMBA vs YANGA MAPEMAAAA….. JANUARI HII TU ‘MBUGI LIINALIA’ TENA…5G KUJIRUDIA?

SIMBA vs YANGA MAPEMAAAA….. JANUARI HII TU ‘MBUGI LIINALIA’ TENA…5G KUJIRUDIA?

Habari za michezo

ACHANA na ile dabi iliyopita ya timu za wanaume za Simba na Yanga, iliyoshuhudiwa Wekundu wakilala 5-1 au ile ya wiki iliyopita ya Ligi Kuu ya Vijana wa U-20 ambayo Wekundu pia walipasuka 4-0, kuna hii ya dabi ya wanawake Yanga Princess na Simba Queens itakayopigwa Januari 03, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Dabi hiyo ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) imekuja zikiwa zimepita wiki kadhaa tu tangu timu zilipokutana kwenye Ngao ya Jamii na dakika 90 kumalizika bila kufungana na penalti zikaamua pambano kwa Simba kushinda 5-4 na kwenda fainali ilikobeba kwa kuifunga pia kwa penalti, timu ya JKT Queens.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake, kocha msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema licha ya kuwa Yanga ina kikosi kizuri lakini malengo yao ni kushinda kila mchezo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa.

Aliongeza, wanafahamiana vizuri na Yanga kwani walikutana kwenye Ngao hivyo hautakuwa mchezo rahisi na anaamini makosa waliyofanya katika mchezo uliopita hawatayarudia kutokana na maandalizi mazuri waliyofanya.

“Tulianza msimu bila ya kufunga mabao ndani ya dakika 90, tumerudi kwenye Ligi tunafunga lakini bado kuna nafasi nyingi za mabao tunazikosa hilo tunalifanyia kazi ili tuepuke makosa yatakayotugharimu baadaye kwa kuwa tunacheza na timu nzuri ambayo nayo inataka matokeo mazuri,” alisema Mgosi.

Kwa upande wa kocha mkuu wa Yanga Princess, Mzambia Charles Haalubono alisema timu yake inapata matokeo mazuri lakini bado haridhishwi kutokana na wachezaji wanavyopoteza nafasi nyingi wanazotengeneza.

“Kikosi changu kinazidi kuimarika siku hadi siku na kinacheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi lakini bado limekuwa tatizo la umaliziaji ambalo ndio asilimia kubwa tunafanyia kazi ili kwenye mchezo wa dabi tusirudie makosa,” alisema Haalubono.

Tangu mwaka 2018, timu hizo zimekutana mara 10, Yanga imeambulia ushindi mara moja mwaka 2022 wa bao 1-0 lililofungwa na Clara Luvanga ambaye sasa anakipiga Al Nassr ya Saudia, Simba Queens imeshinda mechi sita na sare ni tatu.

Hivyo itakuwa ni mechi ya kutaka kuonyesha ubabe kwa timu zote mbili kwani mwaka jana zilipokutana kwenye ligi zilitoka sare ya bao 1-1.

SOMA NA HII  KUHUSU ISHU YA IBENGE KUTUA AZAM FC....AL HILAL WATOA TAMKO RASMI...