Home Habari za michezo UKWELI KUHUSU ‘MZUNGU’ ANAYECHEZA TAIFA STARS….ASILI YAKE NA JINSI ALIVYOPEWA SHAVU LA...

UKWELI KUHUSU ‘MZUNGU’ ANAYECHEZA TAIFA STARS….ASILI YAKE NA JINSI ALIVYOPEWA SHAVU LA AFCON…

Habari za Michezo leo

WAPO ambao wanamwita Jadon Sancho wa Kizimkazi kwa Mama. Huyo ni winga wa boli, Tarryn Allarakhia ambaye amekuwa gumzo nchini kufuatia kiwango kizuri alichokionyesha katika mchezo wa kirafiki wa Taifa Stars dhidi ya Misri ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Fainali za Afrika (Afcon).

Allarakhia aliyezaliwa na kukulia Uingereza ni ingizo jipya katika kikosi cha Stars ambacho kitatupa karata yake ya kwanza ya Afcon, huko Ivory Coast keshokutwa Jumatano kwa kucheza dhidi ya vigogo, Morocco kwenye Uwanja wa San Pedro.

Kasi na maarifa ya winga huyo, viliwavutiwa wadau mbalimbali wa soka waliofuatilia mchezo huo wa kirafiki ambao Stars ilipoteza kwa mabao 2-0. Allarakhia anasubiriwa kwa hamu kutazamwa kwenye mchezo wa michuano hiyo itakayofikia tamati Februari 11.

Akiwa Ivory Coast, Allarakhia anayeichezea klabu ya Wealdstone ya National League England anasema kuichezea Stars ni fahari na anaeleza haikumuwia vigumu kufanya uchaguzi huo. Winga huyo anacheza ligi moja na Haji Mnoga ambaye anaye amezaliwa na kukulia England.

“Mimi na Haji tunafahamia vizuri tu na sote tumechagua njia moja ambayo ni kuichezea Tanzania, najua Watanzania ni watu wenye upendo na wapo nyuma ya timu yao kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mashindano. Kiukweli hakuna ambaye alinishawishi nilipopata nafasi sikuona sababu ya kukataa Tanzania imeona kuwa kuna kitu kwangu,” anasema winga huyo.

Sancho huyo wa Kizimkazi kwa mama kama ambavyo wadau wengine wa soka wanavyomwita atakuwa mchezaji wa kwanza kwa Wealdstone kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika haijawahi kutokea kwa nyota wa klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka 125 iliyopita.

Wealdstone imembebea bango mchezaji huyo kwa kuandika habari zake kila wakati tangu alipoitwa hadi alipocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri na vile ambavyo yupo tayari kuweka historia kwenye klabu yao.

Allarakhia yupo tayari kwa Afcon na anasubiri kwa hamu kucheza fainali hizo kubwa zaidi barani Afrika ambazo zinakutanisha mastaa kibao wakubwa kutoka klabu mbalimbali ambazo zimekuwa zikitikisa Ulaya.

“Tumekuwa na maandalizi mazuri ambayo naamini yatatusaidia kufanikisha kuwa washindani, kama ilivyo kwa timu nyingine na sisi tunanafasi ya kuvuka hatua hii, morali ya timu ni kubwa sana, kila mchezaji nimeona anapambana kwa ajili ya kupata nafasi ya kucheza,” anasema.

Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa fundi huyo wa boli,inaelezwa ushiriki wa Taifa Stars kwenye fainali hizo, ni miongoni mwa mambo ambayo yalimvutia kufanya maamuzi ya kuichezea Tanzania kwani anaamini kuwa Afcon ni jukwaa kubwa ambalo linaweza kumfanya mchezaji kutoka hatua moja kwenda nyingine.

“Alitushirikisha na kujadiliana naye hatukuona kwakweli sababu za kupoteza fursa ya namna hiyo, ni mchezaji mzuri sana, ambaye naamini anaweza kuleta utofauti kwenye timu, ni mzuri kushambulia akitokea pembeni na hata kucheza nyuma ya mshambuliaji kokote ambako kocha atataka kumtumia anaweza kuonyesha,” anasema miongoni mwa washikaji zake wa karibu.

Allarakhia ni mzaliwa wa Redbridge, London. Alianza safari yake ya soka kwenye akademi ya Leyton Orient.

Baada ya kukua na kukomaa kisoka aliwahi kupata nafasi ya kufanya majaribio Bournemouth wakati wa kiangazi cha 2015 na pia alikuwa na majaribio ya wiki moja katika klabu ya Norwich City.

Japo hakupata nafasi ya kusajiliwa na klabu hizo ambazo zimekuwa zikishiriki Ligi Kuu England, fundi huyo alionekana kuwa na kitu kiasi cha kusajiliwa katika kikosi cha kwanza cha Aveley kutoka kwa mfumo wao wa vijana mwaka 2015 ambapo alitumika zaidi kama winga.

Alicheza mechi nane za Ligi akiwa na Aveley kati ya Oktoba na Desemba na akafunga bao moja, na pia akashiriki mara moja katika Kombe la Wakuu la Essex. Januari 2016, Allarakhia akawa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na kocha Steve Ball kwenye kikosi cha Maldon & Tiptree.

Alifunga bao moja katika mechi 18 katika kipindi cha pili cha msimu wa 2015-16, na kufunga mabao manne zaidi katika mechi 37 katika msimu wake wa kwanza kamili akiwa na Jammers.

Katika miezi yake michache ya kwanza katika klabu, alikuwa miongoni mwa wachezaji hatari.

Julai 2017, Allarakhia alitia saini mkataba wa mwaka mmoja na Colchester United, lakini hata hivyo mambo hayakumwendea vizuri kiasi cha kutemwa mwishoni mwa msimu huo. Agosti Mosi 2018, Crawley Town ilimsajili winga huyo kwa mkataba wa miaka miwili.

Alianza kucheza kwa mara ya kwanza Agosti 14 katika mechi ya Crawley ya EFL Cup dhidi ya Bristol Rovers. Baadaye akatolewa kwa mkopo wa muda mfupi kwa Wealdstone lakini hata hivyo uliongezwa. Alicheza mechi 18, akifunga mara 4 huku Wealdstone akifika nusu fainali ya mchujo.

Agosti 19, 2021, Allarakhia alijiunga na timu ya National League, Woking kwa mkataba wa mwaka mmoja kufuatia kipindi kifupi cha majaribio aliyofanya kabla ya kuondoka Julai 2022 baada ya mkataba kumalizika.

Juni 27 2022, Allarakhia alijiunga tena na Wealdstone baada ya kuondoka kwake Woking, alifunga bao lake la kwanza katika klabu Agosti 16, 2022, na kufunga bao la pili katika ushindi wa 2-1 ugenini Oldham Athletic tangu hapo amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu kwenye kikosi hicho hadi sasa.

WASIFU WAKE
Jina: Tarryn Allarakhia
Kuzaliwa: Oktoba 17 1997
Mahali: Redbridge, London, England
Urefu: 5 ft 9 in (1.75 m)
Nafasi: Kiungo, Winga
Klabu: Wealdstone
Jezi: 7

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA ALHAMISI