Yanga ni timu yenye heshima kubwa Tanzania. Huwezi kuwa na maswali mengi ukisikia jina la timu hiyo linatajwa kokote duniani.
Sasa inatafuta ubingwa wa 30 wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa ndiyo timu iliyotwaa ubingwa mara nyingi, lakini ikiwa inatafuta ubingwa wa tatu mfululizo, ni jambo adimu kutokea.
Timu hiyo ambayo imetimiza miaka 89, inaongoza ligi kuu ikiwa imeshacheza nusu ya mechi za msimu huu, lakini ikiwa haina upinzani wa timu yoyote nyuma yake hadi zote zitakazofikia michezo 15 kama yenyewe.
Lakini siyo kwenye pointi tu, Yanga inaendelea kutawala kwenye maeneo yote muhimu kwenye ligi hiyo na hakuna shaka kuwa unaweza kusema hii ndiyo baba lao kwenye soka la Tanzania.
YANGA POINTI 40
Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa imekusanya pointi 40 ambazo hakuna timu inayoweza kuzifikia kwenye ligi hiyo hata kama ina michezo miwili mkononi.
Simba ambayo ina michezo mmoja mkononi, inaweza kufikisha pointi 36 tu endapo itashinda mechi yake iliyobaki dhidi ya JKT Tanzania, lakini Azam iliyocheza michezo 14 itamaliza mzunguko wa kwanza na pointi 35, ikishacheza mchezo wake mmoja wa kiporo.
KMC inayoshika nafasi ya nne, itamaliza kiporo chake kimoja na ikishinda itamaliza mzunguko wa kwanza na pointi 24 tu, msimu uliopita Yanga ilitwaa ubingwa ikiwa na pointi 78, hivyo endapo ikishikilia hapa ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo tena.
YAO KOUASSI 6
Baada ya utawala wa mabeki Shomary Kapombe na Mohammed Hussein wa kuwa vinara wa kupiga pasi zilizozaa mabao, sasa ni dhahiri kuwa staa mwingine ameibuka na kuwafunika.
Yao ambaye ni beki wa pembeni wa Yanga, amekuwa na ubora wa hali ya juu kwenye mzunguko wa kwanza akiwa amepiga pasi tano zilizozaa mabao na kuwa kinara.
Msimu uliopita kwa upande wa walinzi, Kapombe ambaye kwa sasa anazo nne alimaliza akiwa na tano na Tshabalala mwenye tatu alimaliza akiwa na tano pia, ndiyo walitawala kwenye eneo hili, lakini msimu huu akiwa ameongezeka, Lusajo Mwaikenda kutoka Azam mwenye pasi nne, je Yao atatawala na mzunguko wa pili na kuvunja rekodi ya mabeki hao wazawa? Tusubiri.
AZIZ KI MABAO 10
Ni dhahiri kuwa msimu huu unaweza kuwa wa aina yake kwenye nyaja ya ufungaji tofauti na ule uliopita, kiungo wa Yanga Aziz Ki ndiye anaongoza kwenye eneo hili akiwa ameshafunga mabao 10 kwenye michezo 15, ambayo timu yake imecheza.
Ki anakuwa kwenye eneo hilo pamoja na kwamba hajacheza michezo minne ya hivi karibuni, dhidi ya Kagera, Mashujaa, Dodoma na Prisons lakini bado anaonekana kuendelea kutawala kwenye eneo hilo, hivyo ana wastani wa bao moja kwenye kila mchezo ambao amecheza, akirudi anaweza kuwa moto zaidi, lakini anaonekana kuwa anaweza kuvunja rekodi ya ufungaji ya msimu uliopita ambapo, Fiston Mayele na Saido Ntibazonkiza walifunga mabao 17 tu na kuwa wafungaji bora.
DIARRA MABAO: 8
Yanga inakwenda mzunguko wa pili ikiendelea kutawala na rekodi zake za kuwa na safu nzuri ya ulinzi ambayo imekuwa ikiongozwa na Djigui Diarra ambaye amekaa langoni kwenye michezo mingi, mabeki Yao, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Bacca na Joyce Lomarisa, wamemaliza mzunguko kama vinara wa timu yenye safu bora ya ulinzi baada ya kuruhusu mabao nane tu, ingawa msimu uliopita jumla ilifungwa mabao 18, hivyo wastani wa msimu huu ni bora zaidi.
Katika mabao hayo, Diarra anatajwa kuwa kipa aliyefungwa machache zaidi kwenye ligi hiyo kwa kuwa timu hiyo imeruhusu mabao mawili kwenye michezo minne ambayo hayupo langoni, lakini Yanga ina maliza pia mzunguko huu ikiwa kinara wa kufunga mabao na timu hiyo imefunga 36 sawa na Azam FC, lakini yakiwa ni mabao saba mbele ya Simba, hivyo kama Simba inataka kuipiku hapa, ishinde 8-0 dhidi ya Geita Gold.