Home Habari za michezo BAADA YA KUIFANIKISHIA KUTINGA ROBO FAINAL CAF….GSM KABAKI NA DENI HILI TU...

BAADA YA KUIFANIKISHIA KUTINGA ROBO FAINAL CAF….GSM KABAKI NA DENI HILI TU KWA YANGA…

Habari za Yanga leo

Kikosi cha Yanga juzi usiku kilikuwa Kwa Mkapa, jijini Dar es Salaam kikiipambania nafasi ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria na bila shaka matokeo tayari umeshayasikia. Sitaki kusema sana.

Ni wazi kuwa kwa miaka hii mitatu, Yanga imekuwa imara sana chini ya ufadhili wa bilionea, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’. Imeweza kununua wachezaji wakubwa na kuwalipa vizuri. Imeajiri makocha wenye wasifu mkubwa kama Nasredine Nabi kutoka Ubelgiji na sasa Miguel Gamondi wa Argentina.

Mbali na makocha wakuu, imekuwa na benchi la ufundi lenye wataalam wa kutosha. Mambo mengi sasa yangafanyika kisayansi. Imerekebisha miundombinu ya ofisi zake. Inafanya vizuri kwenye soko la jezi.

Ndani ya uwanja imekuwa na mafanikio makubwa zaidi. Imetwaa mataji yote ya ndani kwa miaka miwili mfululizo. Imefika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana ikiwa ni mara ya kwanza katika historia. Kwa kifupi Yanga sasa inaishi katika sayari yake. Sio Simba wala Azam FC zimeweza kuipa ushindani. Na mwaka huu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25 imefika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1998 wakati baadhi ya vijana walioajiriwa sasa hawakuwa hata wamezaliwa.

Wakati Yanga ikiendelea kufanya vizuri bahati nzuri kwao ikawa na kumbukumbu ya kufikisha miaka 89 tangu kuanzishwa kwake. Ni muda mrefu sana. Yanga ilianzishwa wakati Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere akiwa na miaka 12 tu. Ni kitambo sana.

Yanga ikafanya sherehe kubwa sana. Ndio siku ambayo walitangaza kuhamishia ofisi zao rasmi kwenye Makao Makuu ya klabu mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam baada ya ukarabati. Ni wazi, Ofisi zao zimekuwa za kisasa kweli kweli. Wakati wa sherehe hizo ikatoka taarifa kuwa mfadhili wa klabu hiyo, bilionea Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ ataijengea timu hiyo uwanja kama ishara ya kumbukizi ya kutimiza miaka 89. Ni zawadi yake kwa Wananchi.

Ni taarifa ambayo imekuwa na mapokeo makubwa sana huko mitaani. Wananchi wamefurahi kusikia huenda baada ya miaka mingi watakwenda kumiliki uwanja wao wa kisasa. Inafurahisha sana. Yaani ule Uwanja wa Kaunda, uliokuwa ukitumika miaka kibao ya nyuma kabla ya mafuriko kuutibua, utajengwa mpya na wa kisasa pale pale mitaa ya Twiga na Jangwani. Hata hivyo, taarifa hii wala haikunishtua hata kidogo. Kwanini? Subiri nitakueleza.

Kwa miaka mingi sasa kiu ya mashabiki wa Simba na Yanga imekuwa kuona timu zao zinamiliki viwanja. Wameishi katika ndoto hiyo kila siku. Ni ahadi ambayo imewaweka viongozi wengi madarakani katika timu hizo, lakini hadi leo hakuna kilichofanyika. Kuna viongozi wengi wamewahi kuchukua kabisa hatua za kuonyesha nia ya kujenga uwanja, lakini hawakuwahi kuanza hata msingi.

Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji aliwahi kutoa hadi michoro ya namna Uwanja wa Yanga utakuwa. Akaonyesha namna wanaweza kujenga katika eneo la Jangwani uwanja mzuri na wa kisasa.

Kwa miaka yote sita Manji aliyokaa ndani ya Yanga ahadi hii wala haikuwahi kutekelezwa. Kuna wakati aliwapatia Yanga eneo huko Gezaulole, Kigamboni. Hadi leo haifahamiki kama eneo hilo bado lipo ama la.

Kwa Simba viongozi wengi wamekuwa wakitoa ahadi hiyo pia. Angalau Ismail Aden Rage alifanya jitihada za kununua eneo la kujenga uwanja huko Bunju. Hata hivyo eneo hilo lilikaa kwa miaka mingi hadi kuja kuendelezwa.

Wakati Mohamed Dewji anatangaza kuwekeza ndani ya Simba naye aliahidi kujenga uwanja wa kisasa, hosteli na vitu vingine. Nini kimetokea? Hakuna. Tangu Dewji ametangaza kuwekeza Simba ni miaka zaidi ya sita sasa na hakuna kilichoendelea.

Angalau huko Bunju kumekuwa na ule uwanja wa mazoezi ambao ni jitihada zilizoanzishwa na uongozi wa Evans Aveva kabla ya kukamilishwa na Dewji. Hakuna kipya sana. Ni uwanja wa kawaida wa mazoezi tu. Huwezi kutaja kama ni uwekezaji.

Kuna wakati aliyekuwa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez alionyesha jitihada za kuanza kwa mradi huo. Akaenda na Wakandarasi eneo la mradi. Wakafanya vipimo vya ujezi. Sijui viliishia wapi. Hivi majuzi, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema fedha iliyokuwepo imejenga uzio. Ni ajabu na kweli.

Hivyo, taarifa hii ya GSM wala hainishitui hata kidogo. Ni taarifa ambayo tumeisikia kwa miaka mingi. Haina jipya sana. Huu ni mtihani kwake kwa Wanayanga. Akitekeleza atajijengea heshima kubwa, akikawama kama waliokwama wenzake atakuwa amejivunjia. Ujenzi wa uwanja ni jambo gumu kutekelezeka. Kwanini?

Kwanza gharama za kujenga uwanja ni kubwa mno. Uwanja mzuri wa kawaida unahitaji sio chini ya Shilingi 30 bilioni na kuendelea. Fedha hizi zinatakiwa kutolewa wakati maisha mengine ya timu yakiendelea. Yaani timu iendelee kusajili, kulipa mishahara, kufanya shughuli zake za kila siku na mengineyo. Ni ngumu sana.

Kwa msimu uliopita peke yake GSM alitoa karibu Shilingi 5 bilioni kuongeza katika bajeti ya Yanga. Hii ina maana kuwa Yanga bado haijawa na fedha za kujiendesha yenyewe tu kwa shughuli zake za kila siku. Unadhani ni rahisi GSM kuendelea kutoa fedha hizo za uendeshaji na bado akatoa mabilioni ya kujenga uwanja?

Lady Jay Dee aliwahi kuimba akisema Usiusemee Moyo. Acha kwa leo niishie hapo. Siwezi kujua moyo wa GSM unawaza nini. Ila akijenga uwanja kama inayodaiwa ameahidi basi niko palee nimekaa. Mje mniweke ‘Bleach’ kama la Pacome.

SOMA NA HII  YANGA WAJA NA JAMBO HILI JIPYA KWENYE MARUDIANO NA AL MAREKH