Home Habari za michezo SIMBA, YANGA KITAKWIMU ZAIDI….WAKITULIZA ‘MAPEPE KUTOBOA CAF NI EASY’ SANA…

SIMBA, YANGA KITAKWIMU ZAIDI….WAKITULIZA ‘MAPEPE KUTOBOA CAF NI EASY’ SANA…

Habari za Michezo

Wakati wekundu wa Msimbazi, Simba ikijiandaa kujibu mapigo ya watani zao, Yanga wikiendi hii kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, wananchi hao wataelekeza leo, Ijumaa dua zao huko Cairo, Misri ambako kikosi hicho kitakuwa mzigoni kupigania ufalme kwenye kundi D dhidi ya miamba ya soka la Afrika, Al Ahly.

Msimu huu Simba itakuwa ikisaka robo fainali ya nne mfululizo katika michuano ya CAF huku ikiwa ya pili mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu uliopita ilitinga hapo hatua hiyo, kijumla katika michuano hiyo Mnyama ana robo fainali tatu ikiwemo ya 2018–19 ndani ya misimu mitano iliyopita.

Yanga ambao msimu uliopita ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, hii ni awamu yao ya kwanza kutinga hatua ya robo fainali.

Vijana hao wa Miguel Gamondi wanakibarua kizito leo kwenye Uwanja wa Kimataifa pale Cairo, Misri huku jambo zuri kwao ni kwamba hawana chakupoteza katika mchezo huo hivyo wanaweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kuishangaza Al Ahly na kuongoza kundi.

Licha ya Yanga kuwa na takwimu nzuri katika michezo yake ya ugenini, kocha wa zamani wa timu hiyo, Hans van der Pluijm anaamini mpango wa kuwaheshimu unaweza kuwasaadia katika mchakato wa kuwania nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa kundi hilo.

“Hongera kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki kwa hatua ambayo timu imefika, mechi hii inaweza kuwa kipimo kingine kwao kuelekea katika michezo ya robo maana mpinzani wanayeenda kukutana naye hapo baadaye atakuwa kwenye daraja la Ahly, itakuwa mechi nzuri lakini Yanga inatakiwa kuiheshimu Ahly mno huku ikitekeleza mpango wake kwa uangalifu, sote tunafahamu ubora wa wapinzani wao,” anasema.

Kwa upande wake, Luc Eymael ambaye licha ya kwamba hakuondoka vizuri Yanga, ameuchambua mchezo huo huku akisema ushindani ambao timu hiyo imekutana nao kwenye hatua ya makundi mbele ya Medeama, CR Belouizdad na Ahly utawafanya kutokuwa na hofu juu ya timu ambayo watakutana nayo kwenye hatua ya robo fainali.

“Nadhani Yanga wanatakiwa kuwa watulivu wasijipe mlima wa kupanda kwenye mchezo wao wa mwisho, unatakiwa kuwa sehemu ya kujindaa na mechi ya robo maana tayari walishafuzu, ambacho kinatakiwa kuwa akili mwao ni kwamba kila timu iliyotinga hatua hiyo ni bora,” anasema.

Takwimu zinaonyesha katika michezo mitano iliyopita kwa Yanga ikiwa ugenini kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika shilingi imesimama kwani imeshinda mara mbili kwenye raundi ya kwanza na ya pili ambapo ni dhidi ya ASAS ya Djbouti kwa mabao 2-0 pia wakaitandika Al Merreikh ya Sudan kwa mabao 2-0.

Huku pia ikipoteza mara mbili, moja kwa msimu huu ambapo ilifungwa na Belouizdad kwa mabao 3-0 na nyingine ni msimu uliopita ambapo walifungwa na Al Hilal ya Sudan kwenye mchezo wa raundi ya pili, sare moja ya 1-1 dhidi Medeama.

Wakati kwa Yanga shilingi ikisimama kwa mujibu wa rekodi kwenye michezo ya mitano ya mwisho kwenye michuano hiyo, mambo ni tofauti kwa Al Ahly wanarekodi ya ushindi kwa asilimia 95.

Mabingwa hao mara 11 wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wameshinda michezo yao minne iliyopita ikiwa nyumbani ambapo ni dhidi ya ES Tunis (1-0), Wydad Casablanca (2-1), Kedus Giorgis (4-0), Medeama (3-0) aliyenusurika kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo ni mmoja tu ambaye ni Belouizdad iliyotoka suluhu ingawa ilichapwa mabao 4-0 na Yanga Uwanja wa Benjamin Mkapa.

HEAD-TO-HEAD MATCHES

02.12.23: Yanga 1-1 Al Ahly 20.04.16: Al Ahly 2-1 Yanga 09.04.16: Yanga 1-1 Al Ahly 09.03.14: Al Ahly 2-0 Yanga 01.03.14: Yanga 1-0 Al Ahly 04.04.09: Yanga 0-1 Al Ahly 15.03.09: Al Ahly 3-0 Yanga

KWA MKAPA HATOKI MTU

Ushindi wa mabao 6-0 ambao Simba iliupata Jumatano iliyopita dhidi ya TRA ya Arusha kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) utaongeza morali wakati wakisubiri kumaliza shughuli dhidi ya Jwaneng Galaxy huku ikiwa na tahadhari yasije kujirudia yale ya msimu wa 2021/22.

Ilikuwaje msimu huo? Simba ikiwa na faida ya mabao 2-0 ambayo iliyapata Botswana ilikocheza mchezo wa kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy ilijisahau kwa Mkapa na kukumbana na kipigo cha mabao 3-1 ambacho kiliwafanya kushindwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa faida ya bao la ugenini.

Takwimu za michezo mitano iliyopita zinaonyesha Simba ikiwa nyumbani imeshinda mara tatu dhidi ya Horoya kwa mabao 7-0, Wydad Casablanca mara mbili mchezo wa kwanza kwa kwa bao 1-0 mwingine kwa mabao 2-0 huku ikitoa sare mbili dhidi ya Power Dynamos ya Zambia kwa bao 1-1 na ASEC Mimosas kwa bao 1-1.

Jwaneng Galaxy haina rekodi nzuri ikiwa ugenini kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, imepoteza mechi nne kati ya tano ambazo ni dhidi ya Etoile du Sahel (3-2), Vipers (2-1), Orlando Pirates (1-0) na ASEC Mimosas kwa mabao 3-0.

Mabingwa hao wa Botswana wameshinda mchezo mmoja tu wakiwa ugenini ambao ni dhidi ya Wydad Casablanca.

SOMA NA HII  KIKOSI CHA SIMBA DHIDI YA RUVU SHOOTING LEO