Home Habari za michezo “AHMED ALLY KAWAPONZA SIMBA….”

“AHMED ALLY KAWAPONZA SIMBA….”

Habari za Simba leo

Mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Samson Mbangula amesema amefurahi kuitungua Simba na kuipa timu yake pointi tatu za kwanza ugenini mbele ya Mnyama tangu mwaka 2012, lakini akafichua kilichoifanya aitungue timu hiyo ni Ahmed Ally, Ofisa Habari wa Wekundu wa Msimbazi.

Mbangula alifunga mara mbili jana katika pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba lililochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro wakati Prisons ikishinda mabao 2-1 ikiwa ni mara ya kwanza kushinda ugenini mbele ya Mnyama tangu mwaka 2012.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo, Mbangula alisema amefurahi kuitungua tena Simba, lakini akikiri sababu kubwa ya hasira za kuinyoosha timu hiyo imetokana na Ahmed Ally aliyedai ni rafiki yake, lakini aliyeanza kumtania kabla ya mchezo akidai kwamba hawezi kuifunga timu hiyo kama alivyofanya mwaka 2020 alipofunga bao pekee.

Mshambuliaji huyo mwenye mabao saba kwa sasa katika mechi 19 za msimu huu, amesema  kuwa, kabla ya mechi waliwasiliana kwa ujumbe wa maandishi na Ahmed Ally, na kama kawaida ya Ahmed alianza kutoa shombo zake akimtaka wakutane uwanjani Jamhuri Morogoro.

“Mimi na Ahmed ni marafiki tangu akiwa Azam TV, maneno yake ya shombo nayachukulia kama chachu ya kujituma kwa bidii ndio maana niliingia uwanjani kwa nia moja ya kuisaidia Prisons ili kumnyamazisha, japo video yake aliyosema siwezi kuifunga Simba, labda Samson yule aliyekatwa nywele na Delillah, nimekuja kuiona baada ya mechi kumalizika,” amesema na kuongeza;

“Mabeki Henock Inonga, Che Malone, Babacar Sarr, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliowataja kwamba siwezi kuwapita ni wazuri na naheshimu viwango vyao, ila mpira ni mchezo wa makosa, hivyo timu yoyote inaweza ikashinda ama kufungwa.

“Siku mbili kabla ya mechi, nilimtumia ujumbe wa maandishi nikamwambia kaka muuza magari, akanijibu tukutane uwanjani, akaweka kituo kabisa ili nisiendelee na mazungumzo, baada ya hapo nikawa bize na maandalizi ya mechi”.

Mbangula alipoulizwa kama baada ya mechi amewasiliana na Ahmed, amesema; “Itakuwa ngumu kunipokelea simu, ingawa najua anafanya kazi yake, yupo kwa ajili ya Simba, hivyo ni lazima afanye kitu cha kuwapa furaha mashabiki wake, hata sisi msemaji wetu lazima atatupa moyo sisi na siyo wapinzani.”

Amesema mechi dhidi ya Simba ana mabao matatu na ameisaidia timu ya Prisons kuchukua pointi sita (Jamhuri Morogoro 2-1) na (Nelson Mandela, Sumbawanga, 1-0, Oktoba 22, 2020) na langoni kwenye mechi zote alikuwa ni Aishi Manula.

Mbali na hilo, ameulizwa endapo Simba na Yanga ambayo ameifunga bao moja, zikihitaji huduma yake je atakuwa tayari kuvua gwanda lake, majibu yake yalikuwa haya: “Siwezi kuacha ajira yangu ya Jeshi la Magereza kwa sababu ya Simba na Yanga, ninachopigania natamani kucheza timu ya taifa tu,” amesema.

Kipigo cha juzi kwa Simba ni cha pili msimu huu baada ya kile cha Yanga katika Kariakoo Derby ya Novemba 5 mwaka jana, ambayo Wekundu wa Msimbazi walichakazwa kwa mabao 5-1, kikiwa pia ni cha kwanza kwa kocha Abdelhak Benchikha katika Ligi Kuu Bara tangu alipoajiriwa mwishoni mwa mwaka jana kuchukua nafasi ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyetimuliwa baada ya kipigo hicho cha Derby.

SOMA NA HII  KISA MAFANIKIO YA SIMBA SC CAF....JEMEDARI SAID AMLIPUA TENA MANARA...