Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA IJUMAA…CHAMA, NGOMA WAMTIA TUMBO JOTO KOCHA AL AHLY…

KUELEKEA MECHI YA IJUMAA…CHAMA, NGOMA WAMTIA TUMBO JOTO KOCHA AL AHLY…

Habari za Simba leo

Al Ahly imerudi uwanja wa mazoezi wa El Tetsh, jijini Cairo juzi kuendelea na kambi ya maandalizi dhidi ya Simba, lakini kocha wa timu hiyo, Marcel Koller amefunguka kwa mara ya kwanza juu ya ubora wa Mnyama huku akiwataja mastaa watano anaowahofia na kuanza mikakati ya kukabiliana nao Ijumaa.

Watetezi hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wanatarajia kuja nchini kuvaa na Simba katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo itakayopigwa Kwa Mkapa Ijumaa hii kuanzia saa 3:00 usiku kabla ya kurudiana nao jijini Cairo, Aprili 5 kusaka tiketi ya kucheza nusu fainali.

Rekodi ya timu hizo zilipokutana katika mechi sita zilizopita za michuano ya CAF ikiwamo mbili za Ligi ya Afrika(African Football League) na nne za makundi ya Ligi ya Mabingwa, zimemtisha Kocha Koller aliyesema hawaichukulii poa mechi hiyo kwa jinsi Simba ilivyowasumbua Oktoba mwaka jana.

Koller alisema dakika 90 zao ngumu za ugenini ndio kitu wanachojipanga nazo wakitambua wanaenda kukutana na timu ambayo imekuwa ikiwapa changamoto katika mechi sita walizokutana tangu msimu wa 2018-2019.

Koller hajawahi kushinda mbele ya Simba alisema wakati wakijipanga na mchezo huo licha ya majeruhi walionao kuna mastaa watano wa Msimbazi ambao ni lazima watafute namna ya kudili nao katika mechi hizo mbili kuanzia ile ya kwanza itakayopigwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Mkapa kisha kwa marudiano Uwanja wa Kimataifa wa Cairo utakaochezwa Aprili 5.

Kocha huyo ambaye alichukua taji hilo msimu uliopita alisema wakati Ahly inajindaa kwenda kukutana na Simba ugenini lazima iwachunge viungo Clatous Chama, Fabrice Ngoma, Kibu Denis ambao watatakiwa kuhakikisha hawachezi kwa utulivu wao.

Koller akaugeukia ukuta wa Simba pia akiwataja mabeki wawili wa kati Che Malone Fondoh na Henock Inonga kuwa ndio umekuwa ugumu wa ukamilifu wa mashambulizi yao katika mechi mbili za mwisho walizokutana katika michuano mipya ya African Football League (AFL) zilizoisha kwa sare ya mabao 3-3.

“Tunarudi kwenye uwanja uliotunyima matokeo ya ushindi kwenye mechi zilizopita lakini sasa ni wakati wa kwenda kubadilisha hiyo historia, Simba ni timu nzuri inacheza hizi mechi kwa mikakati mikubwa,” alisema Koller ambaye anapokea sio chini ya dola 150,000 kwa mwezi pale Ahly (Sh381 milioni).

“Tunachotaka kurekebisha sasa ni makosa ya kushindwa kulinda uongozi kama ambavyo tulifanya mechi tatu zilizopita, tunatakiwa kutafuta akili mpya ya namna tutaweza kuwa bora eneo la kiungo kuliko wao, wana wachezaji bora sana nakumbuka yule mwenye jezi namba 17 (Chama), 38 ambaye ana nguvu ya kufanya kazi ya kukaba kwa nguvu (Kibu), hata yule jezi namba 6 (Ngoma) anacheza kwa utulivu na akili kubwa,” alisema Koller na kuongeza;

“Ukiwaangalia kwenye ukuta wao wana mabeki wazuri yule namba 29 na 20 (Inonga na Malone) lakini bado nawaamini washambuliaji wangu wakati tutakapoamua kuwa bora katikati ya uwanja tutaweza kufanya kitu kuharibu utulivu wa ukuta wao.”

Katika mechi hizo za AFL zilizoanzia robo fainali Simba na Al Ahly zilifungana mabao 2-2 kisha kutoka 1-1 mjini Cairo na wenyeji wanasonga kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa ni sare ya 3-3. Aidha Koller aliongeza, Ahly inayoshikilia rekodi ya mataji 11 ya

Ligi ya Mabingwa haitakuja uwanja wa Mkapa kuja kujilinda ambapo itatafuta matokeo ya ushindi ili kurahisisha mchezo wa marudiano.

“Ahly sio timu inayohusudu soka la kujilinda, wakati uliopita tulipata shida ya hali ya hewa ikawafanya wachezaji kupunguza kasi lakini sasa pia tutakuja kutafuta ushindi kwenye mchezo huo wa ugenini lakini tukitanguliza umakini wa kucheza kwa tahadhari.”

Habari njema kwa Waarabu hao na mbaya kwa Simba ni kwamba kiungo wao mkabaji Allou Dieng juzi alirejea uwanjani kwenye mazoezi na wenzake baada ya kukosa mechi sita zilizopita kutokana na majeruhi akiwaacha wenzake watano wakiendelea kusikilizia.

Emam Ashour aliumia juzi akiwa na kikosi cha timu ya taifa iliyokuwa ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya New Zealand akitumika kwa dakika 24, ikielezwa ametenguka bega, huku kipa namba moja na nahodha, Mohammed El Shanawy, kiungo Hussein El Shahat na beki wa kati Yasser Ibrahim.

Katika mechi sita zilizopita za Simba na Al Ahly, kila timu imeshinda mechi mbili za nyumbani, Wamisri wakishinda 5-0 na 1-0, huku ikipoteza kwa Simba 1-0 mara mbili Kwa Mkapa mbali na sare mbili za AFL.

Matokeo yaliyopita Feb 02, 2019 Al Ahly 5-0 Simba

Feb 12, 2019 Simba 1-0 Al Ahly

Feb 23, 2021 Simba 1-0 Al Ahly

Apr 09, 2021 Al Ahly 1-0 Simba

Okt 20, 2023 Simba 2-2 Al Ahly

Okt 24, 2023 Al Ahly 1-1 Simba

Mechi zijazo Ijumaa Robo Fainali CAFCL Simba v Al Ahly Saa 3:00 usiku Kwa Mkapa

Marudiano Apr 05, 2024 Al Ahly v Simba Saa 3:00 usiku Cairo, Misri

SOMA NA HII  RASMI YANGA WAMUUZA BANGALA AFUATA NYAYO ZA FEI TOTO..... ATUA HAPA MAPOKEZI YAKE SASA