MKWAJU wa penalti uliopigwa na kiungo mshambuliaji, Clatous Chama dakika ya 72, umeisaidia Simba kupata sare ya bao 1-1 ugenini mbele ya Ihefu katika pambano la Ligi Kuu Bara, ikiifanya timu hiyo kutimiza mechi nne mfululizo bila ushindi na kuongeza presha kwenye Kariakoo Derby itakayopigwa wikiendi ijayo.
Simba imeambulia sare hiyo kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida baada ya awali kucheza mechi tatu nyuma zikiwamo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho (FA) bila kupata ushindi na kuwapa presha mashabiki wa timu hiyo wakati ikikabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Yanga Jumamosi ijayo.
Katika mechi ya kwanza ya Derby iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana, Simba ilikandikwa mabao 5-1 na Yanga, kitu ambacho mashabiki wa Simba hawataki kiwatokee na sare ya jana imewaongeza presha zaidi wao na hata benchi zima la ufundi la timu hiyo inayoshikilia mataji 22 ya Ligi Kuu Bara tangu 1965.
Wenyeji walitangulia kupata bao dakika ya 41 kupitia Mkenya, Duke Abuya aliyepokea pasi murua kutoka kwa Elvis Rupia na kumchenga kipa Ally Salim kabla ya kutumbukiza mpira wavuni kiulaini.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji na Simba kunufaika kwa kupata bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti hiyo ya Chama baada ya Kibu Denis kuchezewa madhambi na Mzambia huyo kufunga bao hilo kabla ya kutolewa kumpisha Willy Onana.
Matokeo hayo yameifanya Simba kusalia nafasi ya tatu na pointi 46, ikishindwa kuipiku Azam yenye 47, huku Ihefu ikiongeza pointi moja na kufikisha 24 ikipanda kutoka nafasi ya 11 hadi ya tisa.
Katika mchezo huo, Simba imeonekana kuwa bora kwenye umiliki wa mpira japo nyota wake walikuwa wavivu kupambana kusaka mpira wakipoteza na kuwaacha Ihefu waliokuwa wanatumia mipira mirefu kutengeneza mashambulizi na kupata kona tano dhidi ya mbili za Ihefu.
KIUFUNDI ZAIDI
Nini unafanya unapokuwa na mpira, nini unafanya unapoupoteza na nini unafanya katika nyakati ambazo wapinzani wanaanzisha mashambulizi kuanzia langoni (Build Up ).
Katika sehemu kubwa ya mchezo wa jana timu zote hazikuanza kuzuia kwenye mstari wa mabeki katika nyakati ambazo mpinzani anajenga mashambulizi.
Simba ilianza kukaba katika mstari wa pili kwa kuutumia muundo wa 4-4-2, na Saido Ntibazonkiza na Freddy Koublan walisimama nyuma ya viungo wa Ihefu na mbele ya mabeki wao, lengo likiwa ni kuzuia pasi zisiende kwa viungo wa Ihefu, hawakutaka kuwabughudhi mabeki kwa maana ya kuwafuata miguuni badala yake walichagua kufunga njia za pasi.
Katika kipindi cha kwanza half spaces (nusu nafasi baina ya mlinzi wa kulia na mlinzi wa kati) ambazo Simba walikuwa wanashindwa kuzifunga ndizo zilizowafanya waende mapumziko wakiwa nyuma na kuwanufaisha Ihefu katika kipindi cha kwanza kisha wakienda mapumziko wakiwa mbele, muda wote ambao Ihefu walikuwa wanashambulia walikuwa wanapeleka mipira yao pembeni ili wazitumie half spaces (nusu nafasi) hasa ya upande wa kulia ambako Shomari Kapombe na Clatous Chama walikuwa wanachelewa kuifunga, mara nyingi wachezaji hawa wawili walichelewa kurudi kila walipopanda mbele kiasi cha kuwaruhusu mawinga wa Ihefu kupokea mipira na kutoa mipira wakiwa huru.
Katika sehemu kubwa ya mchezo, Simba walifanikiwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini bado umakini wao ulikuwa ni mdogo na kiasi cha kupoteza mipira mingi kirahisi kila na wachezaji wa Ihefu walipofanikiwa na kutaka kuiwania mipira.
Kila ambapo Simba hawakuwa na mpira walikuwa wanazuia na muundo wa 4-4-2 lakini kitu ambacho Ihefu walikifanya ni kupiga pasi za juu ili kuivusha mipira kwenye eneo la kiungo kisha idondoke nyuma ya safu ya kiungo ya Simba, halafu wapite muleule katika nusu nafasi ambazo Simba walikuwa hawazifungi.
Tofauti na Ihefu, walikuwa wanafanikiwa kuzuia mawinga wa Simba SC wasikimbie nyuma ya migongo ya walinzi wa Ihefu FC na mara nyingi ambazo walipoamua kufika kwenye matukio ya kuwania mipira walihakikisha wanaipoka na kuanzisha wao mashambulizi.
Vikosi vilivyoanza;
SIMBA: Ally Salim, Henock Inonga, Che Malone, Mohammed Hussein, Shomari Kapombe, Fabrice Ngoma, Kibu Denis, Sadio Kanoute, Freddy Michael, Said Ntibazonkiza na Clatous Chama.
IHEFU: Khomen Abubakar, Fario Ondongo, Benson Mangalo, Mukrim Abdallah, Benjamin Tanimu, Morice Chukwu, Hernest Malonga, Kelvin Naftal, Elvis Rupia, Duke Abuya na Emanuel Lobeta.
MECHI NYINGINE
Katika mechi nyingine, Geita Gold ikiwa nyumbani, Geita imelazimishwa sare ya 2-2 na Mtibwa Sugar iliyoanza kupata bao la kwanza dakika ya 15 kupitia Jimmyson Mwanuke kabla ya wenyeji kuchomoa dakika ya 20 kwa penalti iliyopigwa na Yusuph Mhilu.
Mashaka Valentino ameiongezea Geita bao la pili dakika ya 35 na kufanya hadi mapumziko wenyeji walikuwa mbele kwa mabo 2-1 na kipindi cha pili Mtibwa ilipambana na kuchomoa bao hilo dakika ya 77 kupitia kwa mtokea benchi, Omary Marungu.