Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema walistahili kutwaa taji la Ligi Kuu, huku akisisitiza kwamba kituo kinachofuata ni Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Yanga wametwaa ubingwa wakiwa na mechi tatu mkononi baada ya kufikisha pointi 71 ambazo washindani wake Azam FC na Simba hata wakishinda mechi zao zote zilizobaki hawawezi kufikia.
Akizungumza Gamondi amesema kutokana na aina ya kikosi alicho nacho hawakuwa na timu ya kuwazuia kutwaa Kombe la Ligi Kuu Bara msimu huu na kusisitisha kuwa sasa nguvu zote wanahamishia FA.
“Nililetwa kwa ajili ya kutetea taji na kuifikisha timu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika hilo nimelifanikisha na kuvuka hadi hatua ya robo fainali ambayo nimetolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti,” amesema.
“Najivunia kufundisha timu bora ambayo inauchungu wa mafanikio kwa pamoja tumefanya kazi sahihi siwezi kumtaja mchezaji mmoja mmoja kila aliyepata nafasi ya kuchea alikuwa bora na amehusika kwa namna moja ama nyingine kwenye mafanikio tuliyoyapata.”
Gamondi amesema baada ya kumaliza kazi ya ubingwa wa ligi nguvu zote wamehamishia kwenye mchezo wa nusu fainali utakaochezwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kati ya Yanga na Ihefu FC.
Amesema amekaa na wachezaji na kuwaambia bado wanayo kazi ya kufanya ili kutwaa taji lingine ambalo pia ni muhimu kwake na kubaini kuwa wapo kwenye hali nzuri ya ushindani na kumhakikishia kuwa hilo pia wanalitaka.
“Wachezaji wangu wapo kwenye hali nzuri ya ushindani na wanautamani mchezo wa Jumamosi lengo lao ni kuona wanatwaa taji hilo pia ili kuweka rekodi sawa kwenye ubora walionao na kuuonyesha kwenye ligi,” amesema.
“Haitakuwa rahisi lakini malengo ni kuona tunatumia mbinu sahihi kushindana na wapinzani ili kufikia malengo na nina imani na kikosi nilicho nacho natarajia kuibuka na ushindi mchezo ujao na kusonga hatua inayofuata.”
Gamondi amesema timu yake imekamilika kila eneo kuna wachezaji wazoefu wengi ambao malengo yao ni kuipa timu mafanikio, huku akiweka wazi kuwa hakuna mchezaji ambaye hapendi kutwaa mataji lakini ubora ndio unaamua kama walivyo wao sasa.