KUNA kazi kubwa kwenye safu ya viungo wakabaji wa Simba, akiwemo Mzamiru Yassin na Fabrice Ngoma ambapo ili waendelea kujihikikishia namba kwenye kikosi cha kwanza lazima wafanye kazi haswa mbele ya usajili mpya wa kiungo, Debora Fernandes ndani ya klabu hiyo.
Simba imekamilisha usajili wa kiungo mkabaji huyo kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea klabu ya Mutondo Stars ya Zambia, Debora mwenye uraia pacha wa Congo Brazzaville, anacheza timu ya Taifa ya Gabon.
Usajili wa Debora unaenda kuwapa wakati mgumu viungo waliopo ndani ya kikosi hicho , Mzamiru, Ngoma na Sadio Kanoute kujihakikishia namba ndani ya kikosi cha timu hiyo baada ya msimu uliopita kuwepo kikosi cha kwanza.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu David ambaye amepewa mikanda ya kuangalia baadhi ya mechi ya Simba za msimu uliopita na kuangalia kazi ya viungo hao wawili, Mzamiru, Ngoma, Augustine Okejepha na Debora nani anaweza kupata nafasi ndani ya kikosi cha kwanza.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema Debora anamudu kucheza kiungo mkabaji (namba sita) ingawa anafurahisha zaidi kucheza namba nane.
Amesema ujio wa kiungo huyo unaongeza nguvu katika eneo hilo, anauwezo wa kuzuia na kupiga pasi sahihi kuelekea mbele na kuanzisha mashambulizi.
“Tunaendelea kusuka timu imara kwa ajili ya muda mrefu maana ya usajili wetu umezingatia umri wa wachezaji wanaosajiliwa, kwa kuongeza mtu katika kila idara na kuifanya Simba bora,” amesema Ahmed.
Debora anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa katika idara ya kiungo wa kati baada ya jana mchana kumtambulish Okejepha kuwa ni sehemu ya usajili kwa kuongeza uimara wa kikosi cha Simba kwa msimu ujao wa Mashindano.