Home Habari za Yanga Leo AZIZ KI ASHINDWA KUJIZUIA KISA CHAMA, DUBE NA BALEKE

AZIZ KI ASHINDWA KUJIZUIA KISA CHAMA, DUBE NA BALEKE

Aziz Ki Yanga

MFUNGAJI BORA wa Ligi Kuu ya NBC Stephen Aziz Ki alisema kuongezwa kwa Clatous Chama, Prince Dube na Jean Baleke ni kama kutamrahisishia kazi alizokuwa akizifanya msimu uliopita na wakati mwingine kuigharimu timu.

Yanga mbali na Chama, Dube na Baleke, pia imesajili beki wa kushoto, Chadrack Boka, viungo Duke Abuya na Aziz Andambwile pamoja na kipa Abubakar Khomeiny na Aziz KI anasema mziki huo mpya na wale wa zamani wamezidi kuifanya Yanga kuwa imara zaidi na wapinzani wakae chonjo kwani watachezea sana.

Aziz KI aliyemaliza kama kinara wa mabao wa Ligi Kuu akifunga mabao 21 na kuasisti nane alisema Yanga imefanya usajili mzuri na malengo ya kufanya hivyo ni kuona wanafikia malengo hasa katika Ligi ya Mabingwa Afrika akiamini hata fainali inaweza kufika baada ya msimu uliopita kuishia robo fainali.

“Ni sajili nyingi zimefanyika, lakini nimefurahi kucheza pamoja na Chama, Dube ni wachezaji ambao wameongezeka kikosini kunipunguzia majukumu hasa eneo la ushambuliaji msimu ujao nitakuwa na kazi rahisi japo haina maana kwamba nikipata nafasi sitafunga,” alisema Aziz KI na kuongeza;

“Niliposikia Dube anakuja Yanga nilimtabiria ataibuka mfungaji bora sasa imetimia kazi iliyobaki ni kucheza kwa ushirikiano na kumtengenezea nafasi nyingi za kufunga na kwa upande wa Chama nafikiri kila mchezaji anatamani kucheza naye ni mchezaji ambaye anauwezo mkubwa hasa kutoa pasi za mwisho.”

Aziz Ki alisisitiza amesalia Yanga ili kuendeleza kazi ya kuipambania timu ifikie mafanikio makubwa ziaid na hasa kuvaa medali za Ligi ya Mabingwa baada ya misimu miwili iliyopita kuvaa za Kombe la Shirikisho.

“Maneno yamekuwa mengi kwamba nimebakizwa na mrembo Hamissa Mobetto sio kweli nimebaki kuipambania Yanga ifikie malengo hilo linawezekana hasa ukiangalia usajili uliofanywa na viongozi kazi imebaki kwetu na benchi la ufundi kuona ni namna gani tunafanya vizuri ndani na nje,” alisema Aziz KI na kuongeza;

“Natambua ubora wa kila mchezaji aliyepo kikosini na namna kila mmoja anatamani kuona tunakuwa bora hii inanipa morali ya kuamini kuwa msimu ujao tutakuwa bora zaidi ya msimu uliopita wachezaji waliongezwa wataongeza nguvu na kufanya kile kinachotamaniwa na wengi.”

SOMA NA HII  TP MAZEMBE WAMNYIMA RAHA NABI....AFUNGUKA A-Z JINSI WANAVYOMKONDESHA...