KOCHA wa Simba, Fadlu Davids, amesema bado hawajamaliza kazi ya kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na wanatakiwa kupambana kupata ushindi kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili nchini wakitokea Libya kwenye mchezo wao wa kwanza ambapo ulimalizika bila kufungana, Fadlu, alisema wamemaliza dakika 45 za kwanza na sasa wanajiandaa kwa dakika nyingine 45.
Alisema kimahesabu ni kama Simba wamepata matokeo mazuri kwenye mchezo huo wa kwanza lakini kwake anaona bado kazi haijaisha na kuna jambo la kufanya kuhakikisha wanapata ushindi utakaowapeleka hatua hiyo ya makundi.
“Tunahitaji ushindi, mipango na mahesabu ya mchezo wa kwanza yameishia Libya, lazima tujiandae na kujipanga vizuri kwa mchezo wa marudiano, kwenye mpira hakuna kitu kinachoshindikana,” alisema Fadlu.
Alisema kwenye mchezo huo wa marudiano hawahitaji kukaa nyuma muda wote wa mchezo kwa kuwa kitu pekee wanachokihitaji ni ushindi kwenye mchezo huo.
“Tutaingia na mpango madhubuti wa kuhakikisha tunatengeneza nafasi nyingi, hatutahitaji kukaa nyuma, lakini lazima tuwe makini kwenye ulinzi, kazi haijaisha mpaka baada ya dakika 90 za mchezo wetu wa marudiano.”
“Sitarajii mchezo mwepesi kwa sababu na wao (Al Ahly Tripoli) watakuja kutafuta ushindi au sare yoyote ya magoli, ni jambo ambalo lazima tuwe makini sana, mashabiki waje kwa wingi kuwatia moyo wachezaji wao,” alisema Fadlu.
Kufuatia matokeo ya suluhu ugenini, Simba inahitaji ushindi wowote ili waweze kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa ngazi ya vilabu Afrika.
Mchezo huo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
[…] Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema kwa mchezo wa leo hawana kitu kingine cha kufanya zaidi ya kushinda na kufuzu […]