Home Habari za michezo KISA UHUJUMU UCHUMI…KOCHA WA SIMBA ASOTA RUMANDE MIAKA 2 MFULULIZO…

KISA UHUJUMU UCHUMI…KOCHA WA SIMBA ASOTA RUMANDE MIAKA 2 MFULULIZO…

Habari za Simba

Aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba, Muharami Sultani (40) na wenzake wanaendelea kusota rumande kwa siku 736 kutokana na upelelezi wa shauri linalowakabili kutokamilika.

Sultan na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manane yakiwemo ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, Novemba 21, 2022 na kusomewa mashtaka yao.

Hata hivyo, tangu wafikishwe mahakamani hapo siku hiyo hadi leo Novemba 26, 2024, washtakiwa hao wamefikisha siku 736 sawa na miaka miwili na siku tano wakiwa rumande.

Licha ya upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 71/2022 kutokamilika, pia washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Pia mashtaka ya kutakatisha fedha hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, leo wakili wa Serikali Frank Rimoy aliieleza mahakama hiyo, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo Serikali inaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini, aliahirisha shauri hilo Desemba 10, 2024 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wapo rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana. Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video huku washtakiwa wakiwa rumande.

Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Dar es Salaam, Kambi Zubery Seif; Said Matwiko mkazi Magole na Maulid Mzungu maarufu mbonde (54) mkazi wa Kisemvule, Dar es Salaam ambaye ana undugu na mtuhumiwa Muharami.

Wengine ni John John maarufu Chipanda (40) mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni kuongoza genge la uhalifu shtaka linalowakabiliwa watu wote ambapo inadaiwa tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 katika maeneo tofauti na ndani ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride.

Shtaka la pili inadaiwa kuwa Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 27.10.

Vile vile, Novemba 4, 2023 washtakiwa, Zuberi, Zungu na Mtwiko katika eneo la Kamegele wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 7.79.

Katika shtaka la nne, tano, sita na saba ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi inadaiwa kuwa Aprili 15, 2021 katika wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam alinunua magari manne aina ya TATA yenye jina la Safia Group of Companies LTD huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Katika shtaka la nane inadaiwa kuwa Aprili 20,2021 mshtakiwa Kambi alinunua gari aina ya TATA yenye jina Safia Group of Companies LTD akijua mali hiyo ilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

SOMA NA HII  A-Z JINSI INJIA HERSI ALIVYOWATIMULIA VUMBI SIMBA KWENYE ISHU YA MUDATHIR....