KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema anahitaji kujaza nafasi chache tu za wachezaji kipindi cha dirisha dogo, lakini ni kwa wachezaji ambao wataingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na si wa kuja kukaa benchi.
Fadlu, amekiri kuwa winga wa timu hiyo, Elie Mpanzu ni mchezaji ambaye wataingia moja kwa moja kwenye kikosi kutokana na jinsi alivyomuona tangu siku ya kwanza na kila anavyozidi kufanya mazoezi, anazidi kumshawishi kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.
“Ni kweli nahitaji wachezaji wachache kwenye kikosi changu kipindi cha dirisha dogo la usajili, lakini ni wale ambao wakija wataingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza. Kama watakaa nje basi itakuwa hivyo kwa sababu ya mifumo, kupumzika, au sababu nyingine ya kikosi kipana, lakini si kwa sababu ya kiwango kidogo.
Kuna timu ambazo zina kikundi cha wachezaji wachache wana uwezo ambao wanafanya kazi ya wenzao, wengine viwango vyao ni vidogo, wanabebwa na wenzao, unaweza kuona mapungufu hayo pale wale wa kikosi cha kwanza watakapoumia,” alisema Fadlu ambaye amesifika kwa kuinua viwango vya baadhi ya wachezaji ambao hapo awali walikuwa hawachezi, pia kutumia idadi kubwa ya wachezaji waliosajiliwa msimu huu mpaka sasa.
Alisema ni bora abaki na wachezaji waliopo sasa, kuliko kuletwa wachezaji ambao watakuja moja kwa moja kukaa benchi na kusubiri wenzao waumie ili wacheze.
“Unaona kwa sasa kwenye kikosi changu kuna mtifuano wa kuwania namba, kwa sababu kila mmoja ana kiwango kizuri, wengi wao nimewakuta, lakini wale ambao watasajiliwa chini yangu ni lazima nijiridhishe kuwa kiwango chao ni cha kuichezea timu ya Simba na ana uwezo wa kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza,” alisema.
Akitoa mfano wa Mpanzu, alisema hakuna shaka yoyote kuwa ni mmoja kati ya wachezaji wataoibadilisha Simba kwa kiasi kikubwa kutokana na uwezo wake.
“Huyu jamaa ana uwezo wa kucheza winga zote mbili, ana uwezo wa kucheza nyuma ya mshambuliaji, anaweza kucheza kiungo mshambuliaji, ana kipaji halisi cha mpira mguuni, ukikaa kwenye miguu yake utaliona hilo, anaweza kuhadaa mabeki, ni hatari anapobaki na beki mmoja au wawili, na kikubwa kuliko yote, ana uwezo wa kupiga mashuti makali kutoka mbali.
Ukiangalia mabao yetu mengi tumefunga ndani ya boksi, Mpanzu atakuja kuongeza kitu kikubwa na kama tukipata wengine kama yeye kwenye nafasi zingine tutaimarisha zaidi kwenye kikosi chetu ili kuwa hatari zaidi kwenye michezo ya kimataifa,” alisema raia huyo wa Afrika Kusini.
Tetesi zinadai Simba huenda ikamsajili straika Mganda, Denis Omendi mwenye miaka 30 kutoka Klabu ya Kitara FC ya Uganda, ili kuongeza nguvu safu hiyo ambayo ina Mcameroon, Leonel Ateba na Steven Mukwala pia kutoka Uganda, kiungo mshambuliaji wa Orlando Pirates, Karim Kimviudi raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, pamoja na Abdelhay El Forsy kutoka Klabu ya Renaissance ya Morocco, ambaye anaweza kujiunga na Simba kwa mkopo wa mwaka mmoja.