KUTOKANA na Al Hilal kuwa tayari na tiketi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mchezo ujao ikiwa nyumbani dhidi ya Yanga, iko wazi kwamba wababe hao wa Jangwani ni wao tu sasa kushinda mechi zao mbili zilizobaki na kusonga mbele bila ya kuangalia matokeo ya timu nyingine.
Matarajio ya Yanga kufanya vizuri yanakolezwa na kauli ya kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge, ambaye amesema atakifanyia mabadiliko kikosi chake cha kwanza ili kuwapa nafasi wengine.
Al Hilal ilifuzu juzi Jumapili baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya MC Alger ya Algeria, ambayo iliwafanya wafikishe alama 10. Matajiri hao kutoka Sudan ambao kwa sasa maskani yao yapo Mauritania wamekuwa timu ya kwanza msimu huu kutinga hatua hiyo licha ya kuwa na michezo miwili mbele.
Ibenge, ambaye aliongoza Al Hilal kuifunga Yanga katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi, alionyesha furaha kwa mafanikio ya timu yake, lakini pia alisisitiza kuwa sasa ni wakati wa kubadili mwelekeo kidogo kwa lengo la kutunza nguzvu za wachezaji wake kwa ajili ya kuzisubiri mechi za robo fainali.
“Kwa sasa tunayo nafasi ya kupumzika kidogo na kujiandaa kwa hatua inayofuata. Hatuwezi kupuuza umakini, lakini ni muhimu pia kuhakikisha wachezaji wangu wanakuwa na nguvu za kutosha kwa changamoto kubwa zilizo mbele yetu,” alisema Ibenge.
Kocha huyo aliongeza kuwa, licha ya kufuzu kwa robo fainali, mabadiliko katika kikosi ni muhimu ili kutoa nafasi kwa wachezaji wengine kupata muda wa kucheza, na pia kupunguza mzigo kwa wale ambao wamekuwa wakicheza mara kwa mara.
“Mchezo dhidi ya Yanga utakuwa na umuhimu mkubwa kwao, lakini kwa upande wetu, tunahitaji kujiandaa kwa hali yoyote. Siwezi kujivunia mapema. Wachezaji wangu watahitaji kupumzika kidogo kabla ya mechi zinazofuata,” alisema.
Kwa upande wa Yanga, hali ni tofauti kabisa. Timu hiyo inahitaji kushinda michezo yake miwili iliyobaki ili kufuzu kwa robo fainali, bila kutegemea matokeo ya timu nyingine. Mchezo dhidi ya Al Hilal utakuwa ni kama fainali kwao, kwani ushindi utawaweka katika nafasi nzuri ya kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo, jambo ambalo linawafanya wachezaji wa Yanga kuwa na presha kubwa ya kuonyesha uwezo wao.
Ibenge, ambaye ana uzoefu mkubwa katika mashindano ya kimataifa, akiwemo mafanikio yake na TP Mazembe, alisisitiza kuwa mchezo huo utakuwa na changamoto kubwa kwa Yanga, lakini aliongeza kuwa Al Hilal itakuwa na umakini mkubwa katika kuendeleza makali yao hata baada ya kufuzu.
Hata hivyo, kitendo cha Ibenge kuweka wazi kwamba atabadili kikosi chake cha kwanza katika michezo iliyosalia kwa kuanza dhidi ya Yanga, inaweza kuwa mtego.
Ukiangalia katika kikosi cha Al Hilal, asilimia kubwa ya wanaotokea benchi ndiyo wamekuwa wakibadili matokeo, hilo lilijidhihirisha mchezo wa kwanza walipokutana ambapo mabadiliko ya kipindi cha pili yaliubadili mchezo huo.
Pia katika mabao sita ambayo yamefungwa na Al Hilal, matatu yamewahusu wachezaji waliotokea benchini ambao ni Yasir Mozamil aliyewafunga Yanga, na Jean Girumugisha ambaye amepachika mawili, huku Mohamed Abdelrahman, Guessouma Fofana na Adama Coulibaly wakiwa ni wachezaji wa kikosi cha kwanza waliofunga mabao.
Matokeo ya mechi ya mwisho kati ya Yanga na MC Alger, ambayo itachezwa jijini Dar es Salaam, yatajumuisha uamuzi wa moja kwa moja kuhusu ni nani atakuwa kati ya timu zitakazofuzu maana Waarabu hao nao wanayo nafasi, lakini pia hata TP Mazembe wenye pointi mbili kwa sasa wakiburuza mkia, nafasi wanayo ikitokea wakishinda mechi zote mbili huku Yanga na MC Alger wapoteze zote, hata hivyo hesabu zao ni ngumu zaidi.
Kwa hiyo, vita ya kufuzu robo fainali inaendelea kuwa na mvuto wa kipekee, huku matokeo ya michezo iliyobaki yakielekea kuwa na athari kubwa kwa timu zinazoshiriki. Yanga wanahitaji kushinda na Al Hilal ingawa imefuzu, itakuwa na kazi ya kumaliza hatua hiyo kwa kishindo ikitaka kujihakikishia kukaa kileleni, upande mwingine MC Alger itakuwa ikipambana na hali yake mbele ya TP Mazembe.
RAMOVIC ASHTUKIA MCHEZO
Wakati Ibenge akiyasema hayo, kocha wa Yanga, Sead Ramovic ameliambia Mwanaspoti kuwa, kila timu katika kundi lao inahitaji nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali, hivyo hawatakaa kusubiri huruma ya mtu, anachokizingatia ni kukiandaa kikosi cha ushindani.
“Simuangalii mpinzani ili kuwa bora, napambana kuhakikisha najenga timu yenye ushindani, ninachokifurahia zaidi ni namna timu yangu inavyoimarika na ipo kwenye morali nzuri, hivyo naamini kila kitu kinawezekana kwa kushindana sisi wenyewe kwa kuboresha timu yetu.
“Tunakutana na mabingwa wa ligi kutoka mataifa tofauti na kuna timu ambazo zina uzoefu mkubwa kama juzi tumecheza na TP Mazembe ambayo imeshatwaa mataji ya michuano hii (mara tano), sasa tunajiandaa kukutana na timu nyingine bora na kongwe kwenye michuano hii, hatutakiwi kuangalia nini wanafanya bali kujipanga ili tuwe washindani,” alisema Ramovic ambaye anapambana kufanya kile alichofanya mtangulizi wake Migeul Gamondi kuipeleka Yanga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika alipofanya hivyo msimu uliopita.
Ramovic alisema kujitoa kwa kila mchezaji ndiko kutakakowafanya wasonge mbele kwenye hatua ya robo fainali huku akisisitiza kuwa timu yake ipo kwenye morali nzuri na kila mchezaji anatamani kuona wanafikia malengo kwa kucheza hatua inayofuata.
Akizungumzia suala la timu kwenda Mauritania kwa ajili ya mchezo huo, Ramovic alisema safari itakuwa kesho Jumatano ili kuwahi kuzoea mazingira kabla ya kukabiliana na mpinzani wao Jumapili.
Wakati kocha akifunguka hayo, Yanga tayari imemtanguliza Hafidh Saleh ambaye ni mratibu wa timu hiyo kwenda nchini Mauritania kwa ajili ya kuweka mazingira sawa kabla ya timu hiyo kuwasili huku taarifa zikibainisha kwamba kiongozi huyo ameondoka jana.