KIUNGO mshambuliaji aliyekuwa akifuatiliwa kwa karibu ili kujiunga na Klabu ya Simba kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, Imourane Hassan, raia wa Benin, amerejea nchini Uswizi kujiunga na klabu yake mama ya Grasshopper Zurich, hivyo kuzima ndoto za Wekundu wa Msimbazi kumpata kipindi hiki.
Vyombo mbalimbali vya habari za michezo nchini Benin, vimeripoti kuwa kiungo huyo aliyekuwa akiichezea Loto Popo ya nchini kwao kwa mkopo kutoka Grasshopper, amerejeshwa kwenye timu hiyo huku mwenyewe akionekana kufurahishwa na hatua hiyo.
Habari zinasema kuwa kabla ya kurejea kwenye timu yake, Simba ilikuwa kwenye mazungumzo na mchezaji huyo akiwa na uwezo wa kucheza kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji pia.
Hata hivyo, magazeti kutoka Benin yanasema mbali na Simba ya Tanzania kumwania, Klabu ya Zamalek ya Misri nayo ilikuwa imeshatia mguu kutaka saini yake.
Uwezo alioonesha akiwa na Loto Popo ndio uliyoifanya timu yake iliyompeleka kwa mkopo kumrejesha tena kikosini na kuziacha kwenye mataa timu ambazo zilikuwa zikimtolea macho.
Hivi karibuni, chanzo kilisema tayari Simba ilikuwa imeanza mazungumzo na mchezaji huyo na yalikuwa yakiendelea vizuri.
Tukio hili limejirudia tena baada ya kumkosa Elie Mpanzu kutoka AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambaye alikuwa asajiliwe na klabu hiyo mwanzoni mwa msimu huu, lakini ghafla alitimkia Genk ya Ubelgiji kwa ajili ya majaribio ambayo alifaulu tatizo likawa umri kwani kwa mujibu wa kanuni za mamlaka za soka za huko, kabla Wekundu wa Msimbazi kumnasa katika dirisha la usajili.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alikiri kuwa kuna mapungufu kwenye baadhi ya maeneo na alitaka yaongezewe nguvu ikiwamo beki wa kati, kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji, huku akisema hakuna haja ya kuongeza mshambuliaji wala winga katika kikosi chake kwa sasa.
“Nadhani baada ya mchezo dhidi ya CS Sfaxien, tutakaa na viongozi ili tuangalie ni nini tutafanya kwa ajili ya kuongeza wachezaji wachache kwenye kikosi,” alisema.
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amethibitisha kuwa kwenye dirisha hili dogo la usajili klabu hiyo itatoa na kuingiza wachezaji kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kikosi chao.
“Tuna utaratibu wetu, ni kweli tunahitaji marekebisho, tumeshaingia makubaliano ya klabu zingine kuhitaji wachezaji wao ili kuwasajili kwa ajili ya kutuongezea nguvu na kama tutawakosa tutakwenda sehemu nyingine, muda bado unatosha,” alisema Mangungu.