Home Habari za michezo PAMOJA NA KUJIFUNGA JUZI….CHASAMBI ‘APEWA MBAVU SIMBA’

PAMOJA NA KUJIFUNGA JUZI….CHASAMBI ‘APEWA MBAVU SIMBA’

Habari za Simba leo

MAKOCHA na wachezaji wa zamani wamemkingia kifua winga wa Simba, Ladaki Chasambi kwa kosa lililotokea juzi wakiliomba benchi la ufundi kuzungumza naye na kuendelea kumpa nafasi kucheza kwa sababu ni hazina ya taifa.

Winga huyo chipukizi katika mechi hiyo ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate licha ya kutoa asisti ya bao la kuongoza alijifunga kwa kuisawazishia timu pinzani na mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakongwe hao walisema kilichofanywa na Chasambi ni sehemu ya mchezo na ni kosa ambalo hutokea mara nyingi na kwamba yeye sio mchezaji wa kwanza kufanya hivyo anatakiwa kujengwa kisaikolojia ili aweze kurudi mchezoni.

Mchezaji wa zamani ambaye kwa sasa ni kocha Zubeir Katwila alimpongeza kocha wa Simba, Fadlu Davids kwa kuzungumza mbele ya umati juu ya changamoto iliyotokea na anaamini ataendelea kumjenga kisaikolojia na kumpa nafasi ya kucheza ili aweze kurudi kwenye ushindani.

“Shida iliyotokea mtu wa kumuweka sawa ni kocha akisaidiana na benchi lake la ufundi. Kilichotokea ni makosa ambayo mchezaji yeyote anafanya. Mwalimu kaongea kiufundi Chasambi anatakiwa ajiamini na kumsikiliza mwalimu anamuelekeza nini ili kurudi kwenye ushindani,” alisema Katwila

“Kama atashindwa kumsikiliza kocha atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye ushindani, lakini akisikiliza anachoelekezwa naamini kocha ataendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kuendelea kufanya kazi yake na akipata atapambana kuwafuraisha mashabiki wanaomkataa sasa.”

Alisema anaamini Chasambi ameumia na ana kazi ya kufanya kurekebisha changamoto iliyotokea ambayo anaamini hakufanya kusudi ilikuwa ni bahati mbaya kwake huku akimtupia lawama kipa Mussa Camara kuwa alikosea kwani alikuwa na uwanda mpana wa kudaka mpira ili iweze kuwa faulo angeiokoa timu.

Kocha wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Boniface Mkwasa alisema ni kosa la mchezo hakukusudia kujifunga, na anaamini mpira ulidunda na kumshinda kipa kutokana na kutua kwa kasi eneo ambalo angeweza kuokoa.

“Naamini ata ikitokea leo apewe nafasi ya kurudia kupiga mpira uliosababisha shida hawezi kujifunga tena kinachotakiwa kufanywa ni benchi la ufundi kumsaidia kwa kumjenga na kumpa nafasi ya kuendelea kumuamini kwasababu ni hazina ya taifa,” alisema na kuongeza:

“Chasambi bado ni mdogo anatakiwa kuendelea kufundishwa baga lipi na zuri lipi akipewa nafasi atafanya vizuri, lile ni tukio la kimchezo hapaswi kulaumiwa na yeye ni mwanadamu alikuwa na lengo zuri la kurudisha lakini mpira ulikuwa na kasi na yeye si mtu wa kwanza kufanya hivyo asihukumiwe kama kaua.”

SOMA NA HII  BAADA YA MORRISON KUMTAJA KUWA ANAMFUNDISHA LUGHA YENYE MATUSI...MKUDE AIBUKA NA KUMJIBU HAYA...