Home Habari za michezo ULE MCHONGO WA SIMBA KWA WAARABU HUU HAPA….JE WATARUDIA YA YANGA..?

ULE MCHONGO WA SIMBA KWA WAARABU HUU HAPA….JE WATARUDIA YA YANGA..?

Habari za Simba leo

SIMBA nd’o zetu. Huu ni msemo uliozoeleka kwa mashabiki wa klabu hiyo linapokuja suala la mechi za kimataifa.

Na safari hii ni zamu ya klabu hiyo kuonyesha ukubwa wake katika michuno hiyo wakati ikisaka taji la kwanza la Afrika kupitia Kombe la Shirikisho.

Ndio! Simba ni klabu pekee iliyosalia katika michuano hiyo kutoka Tanzania baada ya Yanga, Azam na Coastal Union za Bara na JKU na Uhamiaji kutoka Zanzibar kuong’olewa hatua tofauti ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Yanga iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa kama Azam na JKU zilizoishia raundi ya awali, ilitolewa makundi wakati Coastal Union na Uhamiaji nazo zilitolewa mapema katika Kombe la Shirikisho ambayo Simba imepenya kucheza robo fainali.

Juzi jioni huko Doha, Qatar ilifanyika droo ya mechi za robo fainali na safari nzima ya ubingwa wa michuano hiyo kwa msimu huu, huku Simba ikipewa Al Masry ya Misri, itakayoanza kwa kuifuata kwao kabla ya kurudiana nyumbani kati ya Aprili 2 na 9, mwaka huu.

Kwa misimu mitano iliyopita Simba ikipenya hatua hiyo katika michuano ya CAF iliishia hapo hapo robo fainali kwa kung’olewa, lakini safari hii ni zamu ya kutaka kuzima ngebe za watani wao wa jadi, Yanga ambayo 2022-2023 iliandika rekodi ya kuwa klabu ya kwanza nchini kufika fainali ya Shirikisho.

Yanga imekuwa ikiwatambia Simba kwa kufika fainali hizo ikilikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria baada ya matokeo ya mwisho yakiwa sare ya 2-2, Yanga ikifungwa nyumbani kwa mabao 2-1 kisha kwenda kushinda jijini Algiers kwa bao 1-0 la penalti ya Djuma Shaban.

Simba iliwahi kucheza fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, michuano ambayo kwa sasa haipo tena baada ya kuunganishwa na ile ya Kombe la Washidi mwaka 2004 na kuzaliwa kwa Kombe la Shirikisho, lakini watani wao hawakubali wakitaka Msimbazi nao wafike fainali ya michuano ya sasa kama wao.

Kutokana na hali hiyo ni wazi, mabosi wa Simba pamoja na wachezaji kwa sasa wanakuna vichwa wakitafuta namna ya kuitoboa hatua moja hadi nyingine ili wafike fainali na ikiwezekana kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kutwaa taji la Shirikisho na kuzima ngebe za Yanga wanaotambia medali ya mshindi wa pili wa michuano hiyo walizonazo majumbani mwao.

YANGA ILIVYOKUWA

Katika droo ya juzi kule Qatar, ni wazi Simba inaonekana ina njia ngumu ya kupita kuisaka fainali kulinganisha na ilivyokuwa kwa Yanga msimu wa 2022/2023.

Wakati Yanga inafika fainali, haikukutana na wapinzani wagumu kulinganisha na inayoweza kukutana na Simba msimu huu na uthibitisho ni nafasi ambazo timu hizo zimekuwepo kwenye chati ya ubora wa klabu ya Shirikisho Afrika.

Msimu wa 2022/2023 Yanga ilianza kukutana na Club Africain ya Tunisia katika play-off kabla ya makundi na kufanikiwa kuitoa klabu hiyo ya Tunisia wakati huo ilikuwa inashika nafasi ya 20 katika chati ya CAF. Katika hatua ya makundi ilipangwa na TP Mazembe ya DR Congo, AS Monastir ya Tunisia na Real Bamako ya Mali na ikamaliza ikiwa kinara wa Kundi D kwa kuvuna pointi 13 kupitia mechi sita.

Ni Mazembe pekee iliyokuwa juu katika chati ya ubora za CAF kwani ilikuwa nafasi ya saba kwa kumiliki pointi 41, huku timu nyingine mbili kwenye kundi hilo, Monastir na Real Bamako hazikuwa na pointi hata nusu katika chati ya ubora wa soka kwa klabu Afrika kuendana na mafanikio katika miaka mitano ya nyuma ya ushiriki katika mashindano ya klabu Afrika.

Katika robo fainali ilikutana na Rivers United ambayo haikuwa katika chati kwa vile haikuwa na pointi yoyote CAF na kuing’oa na ilipotinga nusu fainali ikaumana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambayo nayo ilikuwa na sifa zilizoendana na zile za Rivers United. Katika fainali ikaumanaa na USM Alger ambayo wakati huo ilikuwa inashika nafasi ya 41 katika chati za ubora na wababe hao ambao wapo pia robo fainali msimu huu walibeba ndoo hiyo.

Katika msimu huu, Simba ilianzia raundi ya kwanza kwa kukutana na Al Ahli Tripoli iliyopo nafasi ya 33 ya chati ya CAF na kuing’oa kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 na kutinga makundi ikipangwa Kundi A sambamba na mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Shirikisho, CS Sfaxien ya Tunisia.

Sfaxien, ilikuwa nafasi ya 39 katika chati ya CAF, pia ilikuwapo CS Constantine ya Algeria ambayo haikuwepo kwenye chati ya ubora kwa vile haikuwa na pointi na nyingine ni Onze Bravos ya Angola ambayo nayo ilifanana na Constantine.

Kwenye robo fainali imepangwa kukutana na Al Masry inayoshika nafasi ya 38 katika chati ya ubora wa miaka mitano ya CAF. Simba inakutana na Al Masry kwa mara nyingine katika michuano hiyo baada ya awali kuvaana katika raundi ya pili msimu wa 2018 na Wamisri kuwazidi Msimbai kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini baada ya sare ya mabao 2-2 na ndio msimu timu hiyo ilifika nusu fainali iking’olewa na AS Vita ya DR Congo.

Wawakilishi wa Tanzania waanzia ugenini Aprili 1 au 2, kabla ya kurudiana Kwa Mkapa na iwapo itaingia nusu fainali inaweza kukutana na watetezi wa kombe hilo, Zamalek pia ya Misri ambayo katika chati ya CAF inashika nafasi ya tano.

Ikiwakosa Zamalek, basi huenda ikacheza na Stellenbosch ya Afrika Kusini ambayo ni wageni kabisa wa michuano hiyo na iwapo Mnyama atavuka hapo salama, basi kuna uwezekano wa kukutana ama na RS Berkane ya Morocco inayoshika nafasi ya sita ya ubora wa viwango vya CAF, juu ya Simba iliyopo ya saba.

Pia inawesa kukutana na Asec Mimosas ya Ivory Coast inayoshika nafasi ya 14 kama sio USM Alger, klabu ya 11 kwa sasa kwa orodha ya CAF au CS Constantine pia ya Algeria ambayo haipo katika orodha, ikitegemeana na matokeo ya mechi za timu hizo katika robo na nusu fainali.

Kifupi ni kwamba Simba inatakiwa kukaza buti kwelikweli iwapo inataka kufikia mafanikio iliyofanya Yanga msimu wa 2022-2023, vinginevyo inaweza kuishia njiani na kuwapa watani wao nafasi wa kuwatambia mtaani.

Kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids alisema kuwa yuko tayari kwa changamoto iliyo mbele yao, kwani hatua waliyofikia sio lelemama kwani kila timu inapiga hesabu za kufika mbali katika michuiano hiyo.

“Tulitegemea droo na timu yoyote ambayo tungecheza nayo ingekuwa ni ngumu. (Al Masry) wanafanya vizuri katika Ligi Kuu ya Misri na itakuwa mechi ngumu hasa tutakapokuwa kwao Misri,” alisema Fadlu.

Fadlu anawategemea zaidi nyota walioifikisha timu hiyo hapo ilipo kama Kibu Denis aliyefunga mabao manne msimu huu hadi kufika robo fainali, Jean Ahoua aliyefunga mabao mawili na kuasisti mbili pia na Leonel Ateba aliyefunga maatatu na asisti moja hadi hatua hiyo.

Mbali na hao, lakini Simba ina kikosi cha wachezaji wenye umri mdogo na vipaji vya juu akiwamo kipa Moussa Camara ambaye katika mechi nane za msimu huu za CAF ameruhusu mabao matano, wakati timu ikifunga mabao 11, yakiwamo matatu ya raundi ya pili na manane ile ya makundi.

SOMA NA HII  WAFAHAMU NNJE NDANI WAPINZAI WA SIMBA NA YANGA LIGI YA MABINGWA AFRIKA....