Home Habari za michezo BAADA YA KUMALIZANA NA MOBETTO…HILI HAPA JIPYA LA AZIZI KI HUKO YANGA...

BAADA YA KUMALIZANA NA MOBETTO…HILI HAPA JIPYA LA AZIZI KI HUKO YANGA πŸ‘ŒπŸ‘Œ…

Habari za Yanga leo

SAHAU ishu ya ndoa yake na Hamisa Mobetto. Achana na kitendo cha kusamehe fungate la ndoa na kukipiga katika mechi za Ligi Kuu kama hana chochote alichofanya. Pia jaribu kupotezea umahiri alionao wa kufunga na kuasisti, ila ukweli ni kwamba kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz KI ameshindikana hata kwenye ufungaji wa hat trick.

Ndio! Kama hujui mwamba huyo wa Ouagadougou, kuna jambo ambalo ameibuka nalo na linawahusu mastaa wote wanaokipiga katika Ligi Kuu Bara hivi sasa na wale waliopita miaka ya karibuni.

Ipo hivi, Aziz KI amewafunika mastaa wote wa Ligi Kuu Bara kwa kutupia hat trick nyingi ndani ya misimu mitano mfululizo kuanzia mwaka 2020-2025.

Rekodi zinaonyesha katika misimu hiyo kuna hat trick 24, japo huu wa 2024-2025 haujamalizika, lakini Aziz KI aliongoza wenzake kwa kutupia nne misimu mitatu mfululizo ikiwa ni rekodi pia katika Ligi Kuu kwa miaka ya karibuni.

Hat trick 24 zimefungwa na wachezaji 16 tofauti wakiongozwa na nyota huyo akifuatiwa na mkongwe John Bocco aliyefunga tatu akiwa na Simba kabla ya kutua JKT TZ.

Mfungaji Bora huyo wa msimu uliopita, Aziz KI alimaliza na mabao 21 na asisti nane kiasi cha kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora (MVP), alisajiliwa na Yanga misimu mitatu iliyopita akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast na misimu yote hiyo tangu atue nchini jamaa ametupia hat trick nne.

Aziz KI aliyefunga mabao matano na asisti saba hadi sasa katika ligi, alianza msimu wa kwanza wa 2022-2023 kwa kufunga hat trick moja katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Kagera Sugar kabla ya uliofuata wa 2023-2024 kupiga mbili katika michezo miwili tofauti dhidi ya Azam FC wakati wakiinyoosha mabao 3-2 kisha akatupia kwa Tanzania Prisons iliyolala 4-1 akifunga mabao matatu.

Msimu huu mwamba huyo ameshafunga hat trick moja kati ya mbili zilizopo katika Ligi Kuu, akifunga siku walipoinyoa KMC kwa mabao 6-1, huku nyingine iliyokuwa ya kwanza imefungwa na Prince Dube pia wa Yanga wakati timu hiyo ikiichapa Mashujaa mabao 3-2.

Hat trick dhidi ya KMC, imemfanya Aziz KI kuvunja rekodi aliyokuwa akiishikilia nahodha wa zamani wa Simba, Bocco aliyekuwa akiongoza kwa hat trick nyingi (3) ndani ya misimu hiyo mitano.

Bocco anayeshikilia pia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 155 kupitia misimu 17 mfululizo akivunja iliyokuwa inashikiliwa na Mohammed Hussein β€˜Mmachinga’ ya mabao 153 aliyoiweka kupitia misimu 13, alifunga hat trick hizo akiwa Simba.

Bocco anayemiliki mabao mawili katika ligi msimu huu, alifunga hat trick hizo tatu ndani ya misimu miwili tofauti kati ya mitatu zilizomfanya sasa awe nyuma ya Aziz KI akianza na dhidi ya Coastal Union 2020-2021 walipowazamisha Wagosi mabao 7-0.

Msimu uliofuata wa 2021-2022 mkongwe huyo alitoka kapa bila kufunga hat trick kwani alimaliza na mabao matatu tu msimu mzima. Hata hivyo, Bocco alizinduka msimu wa 2022-2023 kwa kufunga hat trick mbili sawa na alizokuwa nazo Saido Ntibazonkiza aliyekuwa akicheza naye Simba aliyojiunga nayo akitokea Geita Gold aliyeibuka mfungaji bora sambamba na Fiston Mayele aliyekuwa Yanga kila mmoja akifunga 17.

Hat trick hizo mbili za Bocco alizifunga dhidi ya Ruvu Shooting waliyoinyoa mabao 4-0 na kufanya hivyo tena wakati wakiizima Tanzania Prisons kwa mabao 7-1 ambapo pia Saido alitupia hat trick ya kwanza msimu huo kabla ya kuongeza nyingine walipoizima Polisi TZ kwa 6-1. Saido kwa kufunga hat trick mbili ndani ya msimu mmoja ilimfanya aingie katika orodha ya wachezaji wanaoshika nafasi ya tatu nyuma ya Aziz KI na Bocco kwa kufunga hat trick nyingi sambamba na Jean Baleke aliyekuwa Simba na Prince Dube aliyetupia kupitia Azam na Yanga.

Baleke aliyeitumikia Yanga msimu huu kabla ya kutemwa dirisha dogo alifunga hat trick 2022-2023 akiizamisha Mtibwa Sugar kwa mabao 3-0 na kurudia tena 2023-2024 Simba ilipoiua Coastal Union pale Mkwakwani pia kwa mabao 3-0.

Kwa upande wa Dube alifunga hat trick ya kwanza akiwa Azam msimu wa 2022-2023 wakati wakiizima Polisi Tanzania mabao 5-0 na kurudia tena msimu huu akiwa Yanga walipoiua Mashujaa kwa mabao 3-2 pale KMC Complex.

Wengine waliofunga hat trick moja kila mmoja ni Adam Adam alipokuwa na JKT Tanzania, Juma Liuzio enzi za Mbeya City, Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons, Shiza Kichuya enzi akiwa na Namungo, Ibrahim Ali Mkoko pia wa Namungo na Idris Mbombo aliyekuwa Azam.

Pia wamo Mayele alipokuwa Yanga, Feisal Salum β€˜Fei Toto’ wa Azam, Kipre Jr aliyekuwa pia Azam, Wazir Junior aliyekuwa KMC na Ismail Mgunda enzi akiwa na Ihefu (sasa Singida Black Stars). Mgunda kwa sasa yupo AS Vita ya DR Congo, wakati Wazir Junior anakipiga huko Irak.

SOMA NA HII  WANAOKUSHANGILIA WATAKUJA KUKUCHEKA...KIUNGO SIMBA AMSHAURI FEISAL SALUM "FEI TOTO"