Home Habari za michezo KWA HILI LA JOSHUA MUTALE HUKO SIMBA …..HAYA YATARAJIWE WAKATI WOWOTE ULE….

KWA HILI LA JOSHUA MUTALE HUKO SIMBA …..HAYA YATARAJIWE WAKATI WOWOTE ULE….

HABARI ZA SIMBA-MUTALE

MAISHA yanakwenda kwa kasi na mambo yanabadilika kila wakati leo hii stori ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Joshua Mutale imezima ghafla.

Wakati anasajiliwa msimu huu akitokea Power Dynamos ya nchini kwao Zambia akisaini mkataba wa miaka mitatu, baadhi ya mashabiki wa timu hiyo waliamini wamepata bonge la mchezaji atakayewasumbua mabeki wa timu pinzani kwa chenga na kasi.

Kisha wakampatia jina ‘SGR’ akifananishwa na treni ya kisasa ya mwendokasi, lakini kwa sasa nyota huyo ni kama mambo yameanza kuwa magumu upande wake tofauti na wakati anatambulishwa akitajwa kuwa mchezaji atakayekuja kuisaidia Simba.

Mashabiki walikuwa na hamu ya kumuona na kujua yaliyomo yamo, kwani soka ni mchezo wa hadharani yaani kila mtu anaona kama boli lipo au la.

Msimu ulipoanza Mutale alipewa nafasi, lakini kiwango chake hakikuwa kinawavutia wengi kiasi ambacho ilionekana hatakuwa na maisha marefu ndani ya kikosi hicho kilichosheheni nyota wengi wakali hivi sasa.

Baada ya kutoonyesha kile kilichotarajiwa na wengi nyota huyo alianza kukaa benchi na nafasi yake ikakamatwa na wazawa Edwin Balua na Ladack Chasambi.

Tangu hapo mambo yalianza kuwa magumu kwake na ndani ya nusu msimu Mutale akapata majeraha mara tatu na kumfanya akae jukwaani na kushuhudia timu ikicheza. Baada ya majeraha ilielezwa vigogo wa timu hiyo walipanga kumuonyesha mlango wa kutokea dirisha dogo lililopita, ili nafasi yake ichukuliwe na mchezaji mwingine, lakini akaendelea kusalia kikosini.

ALIVYOZIMA MATARAJIO

Usajili wa Mutale ndio uliovuma wakati wa dirisha kubwa la usajili kutokana na baadhi ya mashabiki wa Simba walimuona nyota huyo akikiwasha na timu yake ya zamani, Power Dynamos kwa Mkapa.

Mchezaji huyo anayecheza pia winga alipokuwa Dynamos ya nchini kwao Zambia alikuwa na kiwango bora hasa mechi za kimataifa ambazo msimu juzi alikuja kucheza kwa Mkapa akiwa na timu hiyo na kutokana na sifa hizo Simba ilimsajili na akaanza kuvuma kabla hata hajacheza mchezo wowote akawa supastaa ghafla.

Nyota huyo ambaye ana kasi ameishia kupoteza mipira anapokuwa uwanjani na uwezo wake wa kufunga umetoweka jambo lililowafanya baadhi ya viongozi kuanza kukuna vichwa, huku mashabiki wakimpotezea.

Hadi sasa ndani ya Simba, mchezaji huyo amecheza mechi 10 kwa dakika 438 katika Ligi Kuu Bara na mbili za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya SC Sfaxien akicheza 27 na Bravos 29. Katika mechi hizo Mutale hajafunga bao lolote.

MPANZU, CHASAMBI

Katika eneo analocheza Mutale wapo nyota kadhaa kama Elie Mpanzu aliyetambulishwa Msimbazi wakati wa dirisha dogo akitokea AS Vita, Chasambi, Kibu Denis na Balua.

Mpanzu tangu ajiunge na Simba amekuwa akipata nafasi mara kwa mara na kuibua vita mpya ya mawinga mbele ya Balua na Mutale ambao wanaonekana kuwa na kibarua kigumu mbele ya Mkongomani huyo.

Tangu atue Msimbazi Septemba 2024, Mpanzu amecheza mechi saba za Ligi Kuu kwa dakika 528 na tayari amemfikia Mutale kwa mabao akifunga moja na asisti moja.

Mchezaji huyo na Chasambi chini ya kocha Fadlu Davids kwa sasa wamekuwa wanaanza pamoja kwenye kikosi cha Simba jambo linalokwenda kumpa wakati mgumu Mutale.

Japo ni mapema sana kumuelezea winga huyo machachari, lakini anapaswa kukaza buti kutokana na wanavyoonyesha viwango wenzake wakimuaminisha Fadlu wanaitaka nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Mutale amecheza nusu msimu, lakini ikumbukwe amesaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Simba hadi 2027, hivyo ana muda wa kubadilika.

ZAMBIA ALIKOTOKA

Mutale aliitumikia Power Dynamos kwa misimu mitatu kabla ya Simba kuvutiwa naye na wakati huo alikuwa na kiwango bora.

Msimu 2021/22 kwenye michezo mitano aliyocheza alifunga mabao matano ilhali uliofuata akacheza mechi tano na kufunga mabao matano wastani wa bao moja kwa kila mchezo.

Msimu uliopita alicheza mechi saba na kufunga mabao manane yaliyomfanya afikishe jumla ya mabao 18 ndani ya misimu mitatu. Kwa sasa zimesalia mechi 10 kumaliza msimu wa 2024/25 na Mutale kama atapata ana kazi ya kuushawishi uongozi na mashabiki wa Simba kwamba anastahili kuendelea kubaki Msimbazi dirisha lijalo.

ALIKWAMA HAPA

Mutale tangu alipotoka Zambia alikuwa na takwimu nzuri kwa kufunga mabao manane katika mechi saba ikiwa ni wastani wa kufunga bao moja kwa kila mchezo.

Ndani ya misimu mitatu aliyocheza Dynamos kuanzia 2021/22, alicheza mechi 17 na kufunga mabao 18 jambo ambalo hadi sasa hajaweza kufanikisha.

Katika Ligi Kuu Bara inawezekana ugeni wa michuano inayotajwa kuwa namba nne kwa ubora Afrika umempa ugumu winga huyo wa timu ya taifa ya Chipolopolo kutokana na kukumbana na nyota wengi wa kimataifa.

Miaka ya hivi karibuni Ligi Kuu Bara imekuwa ikitajwa Afrika kama yenye ushindani mkubwa kutokana na timu za Simba iliyocheza robo fainali ya michuano ya CAF mara sita na Yanga iliyofika hadi fainali Kombe la Shirikisho 2022, kuwa chachu ya nyota wengi kuja nchini.

Sababu nyingine inaweza kuwa presha kubwa Simba ambayo ina mashabiki wengi tofauti na Dynamos na huenda Mutale anashindwa kuimudu.

Vilevile inaweza kuwa presha ya kutaka kufanya mambo makubwa ili kuwaridhisha mashabiki wa timu hiyo waliomuamini tangu anafika, na badala yake anaishia kutofanya anachotaka.

Jambo hilo si geni nchini kwani hata nyota wa Yanga, Prince Dube miezi michache nyuma aliwahi kupitia alipokuwa akikosa mabao kiasi cha kuondoka mitandaoni ili kujaribu kuepusha presha hiyo.

NINI AFANYE?

Kwanza Mutale bado mdogo na umri wake unaruhusu kufanya vitu vikubwa ambavyo viliwahi kushuhudiwa akiwa na Dynamos, lakini anachopaswa kufanya ni kupunguza presha na kujipunguzia majukumu, jambo linaloweza kuwa na faida.

Vilevile aachane na fikra za urithi wa Clatous Chama ambaye alifanya makubwa akiwa na Simba kwa kuangalia namna nzuri ya kurudi mchezoni.

Ndani ya Simba mchezaji huyo ana misimu miwili na nusu ya kucheza, hivyo bado ana muda ingawa Simba na Yanga hazina uvumilivu wa kumsubiri mchezaji hususan mashabiki ambao kwao ni matokeo mazuri na si kingine wanaweza kukutungua muda wowote.

Bahati iliyoje kwake kwani kocha wa Simba, Fadlu Davids licha ya kukosa mabao, lakini anaendelea kumtumia ikionyesha ni namna gani anaamini vipaji vya vijana wadogo akiendelea kumpa muda ipo siku atafanya makubwa akiwa na uzi wa Mnyama.

Sio tu kwa kocha hata viongozi wa timu hiyo wanafahamu uwezo wake, jambo lililofanya pengine asiondolewe dirisha dogo lililopita wakimpa muda wakiamini anaweza kubadilika na kuwapa matokeo uwanjani.

SOMA NA HII  ILI SIMBA AWE BINGWA MSIMU HUU NI KIBU NA AHOUA TU... TAKWIMU ZAO HIZI HAPA....