Home Habari za michezo TRY AGAIN ALIVYOONGOZA ‘UJASUSI’ SIMBA WAKIMVAA MWARABU KESHOKUTWA…

TRY AGAIN ALIVYOONGOZA ‘UJASUSI’ SIMBA WAKIMVAA MWARABU KESHOKUTWA…

Habari za Simba

UONGOZI wa Klabu ya Simba umeanza maandalizi mapema kwa ajili ya mchezo wao wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, utakaochezwa Aprili 2, 2025, nchini Misri.

Hatua hiyo imekuja baada ya mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah Try Again, kutembelea Misri hivi karibuni kwa ajili ya maandalizi ya awali.

Akiwa nchini humo, alifika katika Ubalozi wa Tanzania ili kujadiliana na Balozi kuhusu ujio wa timu hiyo kwa ajili ya mchezo huo muhimu.

Akizungumzia ziara yake, Try Again amesema walipata nafasi ya kubadilishana mawazo na maafisa wa ubalozi, wakijadili maandalizi ya timu itakapowasili Misri.

“Nilikutana na Balozi na maafisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Misri kwa lengo la kujadili maandalizi ya awali. Balozi amenihakikishia kuwa wameweka mipango madhubuti ya kuipokea timu yetu, jambo linalotupa matumaini makubwa ya maandalizi mazuri na mazingira bora kwa wachezaji wetu,” alisema Try Again.

Mbali na maandalizi ya mapokezi, uongozi wa Simba unaendelea kuhakikisha timu inakuwa katika mazingira bora kwa ajili ya mchezo huo. Pia, wamechukua hatua za kumpatia kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids, video za mechi zilizopita za Al Masry ili kujifunza mbinu za wapinzani wao.

Kwa upande wake, kocha wa Simba, Fadlu Davids, ameonyesha furaha kwa namna wachezaji wake wanavyoendelea kuimarika, lakini ameweka wazi kuwa wana kazi kubwa mbele yao.

“Tumefanya vizuri katika mechi za nyumbani, lakini sasa tunakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Al Masry, timu yenye wachezaji wazuri na wazoefu katika mashindano haya. Tunapaswa kuboresha baadhi ya mambo ili kuhakikisha tunakuwa tayari kwa mchezo huo,” alisema Fadlu.

Kwa mujibu wa kocha huyo, kikosi cha Simba kitaendelea na maandalizi kuhakikisha wanapata matokeo mazuri dhidi ya Al Masry na kusonga mbele katika michuano hiyo ya kimataifa.

SOMA NA HII  KISA RUVU SHOOTING KUFUNGWA NA YANGA...RAGE 'AJING'ATA ULIMI'... AFUNGUKA A-Z KILICHOTOKEA...