Home Habari za michezo SAKATA LA WACHEZAJI KUPEWA URAIA WA TZ …HUKUMU YA MAHAKAMA KUU HII...

SAKATA LA WACHEZAJI KUPEWA URAIA WA TZ …HUKUMU YA MAHAKAMA KUU HII HAPA ….

Habari za Michezo leo

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imeitupa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Wakili Peter Madeleka kupinga uamuzi wa Serikali kuwapa uraia wa Tanzania nyota watatu wa timu ya Singida Black Stars.

Nyota hao ni Emmanuel Keyekeh, raia wa Ghana; Josephat Bada (Ivory Coast) na Muhamed Camara (Guinea).

Uamuzi wa kuitupa kesi hiyo ulitolewa na Jaji Evaristo Longopa wa Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dodoma, baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowekwa na wajibu maombi wakiwamo nyota wawili wa timu hiyo.

Alipotafutwa na gazeti hili baada ya shauri hilo kutupwa na mahakama, Madeleka alisema: “Nimepokea uamuzi wa Mahakama. Kwa vile imeondolewa katika hatua ya pingamizi, inatoa fursa ya kujipanga, kurekebisha dosari na kuirudisha.”

Madeleka aliyewakilishwa kortini na Wakili John Seka alifungua kesi pamoja na mambo mengine akiiomba mahakama itamke kuwa uamuzi wa kuwapa uraia nyota hao watatu ulikiuka Katiba ya Tanzania.

Katika uamuzi alioutoa Aprili 9, 2025 na nakala yake kupatikana katika tovuti ya Mahakama jana Aprili 11, 2025, Jaji Longopa alisema pingamizi za awali zilizotolewa na wahojiwa zina mashiko na zinastahili kuzingatiwa.

“Katika mazingira, ombi mbele ya mahakama hii halifai kwa sababu ya kasoro iliyoonekana kulingana na uchambuzi. Kwa sababu hiyo, ni fursa kwa Mahakama kutupilia mbali ombi hilo kwa kuwa na dosari isiyotibika,” alisema jaji.

Shauri hilo la kikatiba lilikuwa dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani kama mdaiwa wa kwanza, Kamishina Jenerali wa Uhamiaji (CGI), mdaiwa wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mdaiwa wa tatu.

Pia nyota hao watatu waliunganishwa kama wajibu maombi wa 4, 5 na 6 mtawalia. Wengine walioshtakiwa ni Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji waolikuwa wadaiwa wa saba na nane mtawalia.

Katika maombi yake, Wakili Madeleka alikuwa anaiomba Mahakama itamke kinga aliyopewa Waziri wa Mambo ya Ndani kupitia kifungu cha 23 cha Sheria ya Uraia, haiendi mbali na kufikia hatua ya kukiuka Katiba na kifungu cha 9 cha sheria ya uraia.

Aliiomba Mahakama itamke kuwa kwa kupendekeza wachezaji hao wapewe uraia, CGI na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji walikiuka Katiba na sheria ya uraia. Pia aliomba Mahakama itamke kuwa kuwapa uraia wachezaji hao Waziri wa Mambo ya Ndani alikiuka ibara ya 26(2) ya Katiba na kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Uraia Tanzania.

Madeleka vilevile aliomba Mahakama itamke kuwa wachezaji hao hawana sifa ya kupewa uraia na kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani, CGI na wachezaji hao kwa pamoja walishiriki kughushi au kutoa uraia katika mazingira yasiyokubalika.

Aliomba Mahakama itoe amri kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na CGI kutaifisha mara moja vyeti vya uraia walivyopewa wachezaji hao na kuwaamuru kusalimisha vyeti hivyo kwa Msajili wa Mahakama wakati hukumu ikisubiriwa.

Madeleka aliomba Mahakama imwamuru AG kama mshauri mkuu wa Serikali kuchukua hatua stahiki zitakazowezesha ‘kumulikwa’ kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, CGI na Mkurugenzi wa Uhamiaji na walio chini yao.

Aliiomba Mahakama imwagize DPP kuanzisha uchunguzi kuhusu vitendo na ushiriki wa Waziri wa Mambo ya Ndani, CGI, wachezaji hao na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji kuona kama jinai yoyote ilitendeka na kuchukua hatua.

Hakuishia hapo, aliiomba itoe amri kwa waziri, CGI na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji kulipa Sh500 milioni kama fidia ya adhabu kwa matendo yao ambayo hayakuzingatia Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977. Kama haitoshi, aliiomba Mahakama iwaamuru wachezaji hao kulipa Sh200 milioni kama fidia ya adhabu ya kufanya matendo yanayokiuka Katiba. Pia wadaiwa walipe gharama za kesi na mahakama itoe amri yoyote inayoona inafaa.

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  PABLO ASHINDWA KUJIZUIA SIMBA...AFUNGUKA KWA 'HASIRA' WACHEZAJI WANAVYOMKAMISHA..HAWANA UBORA..