Home Habari za michezo ALICHOKISEMA FADLU BAADA YA SIMBA ‘KUNYONGWA CAF’ JUZI….

ALICHOKISEMA FADLU BAADA YA SIMBA ‘KUNYONGWA CAF’ JUZI….

Habari za Simba leo

SIMBA imeumia. Mashabiki wamebeba majonzi. Viongozi wamesalia na maswali. Lakini katikati ya huzuni hii nzito, moto mpya unawashwa Msimbazi. Moto wa mageuzi. Moto wa kulipiza kisasi kwa njia ya mafanikio katika michuano ya CAF kwa msimu ujao wa 2025-2026.

Hii imetokana na Simba kupoteza nafasi ya kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya RS Berkane ya Morocco, licha ya kutoka sare nyumbani. Simba ilipoteza ugenini kwa mabao 2-0 hivyo kufanya matokeo ya mwisho kuwa kipigo cha mabao 3-1 na kuwanyima taji Wekundu hao kwa mara nyingine baada ya awali kulikosa Kombe la CAF katika fainali dhidi ya Stella Abdijan ya Ivory Coast.

Kutokana na kukwama kuandika historia, benchi la ufundi, limewatuliza wanasimba kwa kuwaambia kuwa, wanaenda kujipanga upya na kurudi katika michuano hiyo msimu ujao wakiwa imara zaidi.

Simba tayari imeshakata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ikiwa na uhakika wa kumaliza nafasi mbili za juu za Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kuikosa michuano hiyo na kuangukia Kombe la Shirikisho kutokana na kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya msimu uliopita.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids hakuficha maumivu aliyonayo alipozungumza na moja ya gazeti la michezo nchini kwa sauti nzito yenye mchanganyiko wa uchungu na matumaini na kuwatia nguvu Wanasimba.

“Tumepambana hadi mwisho. Tulikuwa na ndoto kubwa. Lakini mpira unafundisha. Sasa tunarudi nyuma kidogo… si kwa ajili ya kukata tamaa, bali kuchaji upya. Lazima tuwe tofauti msimu ujao,” alisema Fadlu anayekuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuifikisha Simba fainali ya michuano ya CAF.

Kocha huyo amesema wanaenda kujipanga na kutumia changamoto walizokutana nazo msimu huu kama njia ya kurudi kwa kasi na kufika mbali katika michuano hiyo ya kimataifa.

Na kweli, tofauti hiyo inaanzia katika meza ya mipango. Tayari uongozi wa klabu kwa kushirikiana na benchi la ufundi umeandaa ramani ya usajili ramani inayoonesha bayana kuwa Simba haitaki tena kuwa mshiriki wa kawaida barani Afrika, bali bingwa halisi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu, Simba inatarajia kufanya usajili makini wa wachezaji watatu hadi wanne wa daraja la juu, wakilenga zaidi ubora kuliko idadi. Kiungo wa namba 10 ni kipaumbele.

Ingawa Charles Jean Ahoua ameonesha kiwango kizuri, bado Simba wanahitaji mchezaji mwingine mbunifu, mwenye uwezo wa kusukuma mashambulizi, kutoa pasi za mwisho na kuamua matokeo kwa akili na ufundi.

“Tunamheshimu Ahoua, lakini ili tuwe timu ya kutisha Afrika, hatuwezi kumtegemea mtu mmoja tu kwenye ubunifu. Tunahitaji mbadala wake, mshindani wake, au mshirika wake. Tunahitaji silaha zaidi,” alisema mmoja wa viongozi wa juu.

Lakini kabla ya ndoto za Afrika, kuna kazi ambayo Simba inatakiwa kuifanya kwenye mashindano ya ndani kabla ya mapumziko kisha maandalizi ya msimu ujao.

Simba sasa inajielekeza kikamilifu katika Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA). Katika ligi, Yanga inaongoza kwa pointi 73, Simba ikifuata kwa pointi 69 huku ikiwa na mechi moja mkononi.

Ushindi katika mechi hiyo ya kiporo unaweza tofauti ya pointi baina yao na Yanga huku kukiwa na mechi moja kati yao katika raundi tatu zilizopita.

Katika Kombe la FA, Yanga tayari imeshafuzu fainali. Simba yenyewe inakibarua kutoka kwa Singida Black Stars mwishoni mwa mwezi huu.

Ushindi kwenye nusu fainali hiyo utafungua ukurasa mwingine wa dabi ya fainali mechi ya heshima na ya kulipiza kisasi.

Katika vikao vya ndani, viongozi wa Simba wameweka bayana dhamira yao:

“Tunajenga kikosi cha fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, si cha Kombe la Shirikisho tena. Tumejifunza. Tumetambua mapungufu yetu. Na sasa tunarudi kwa kasi kubwa zaidi.”

Mashabiki nao wameanza kurejeshewa matumaini. Kauli ya “Subirini muone Simba hatari zaidi si ya kutupwa hewani ni ahadi. Ni kiapo. Ni onyo kwa wapinzani ndani na nje ya nchi.

Msimu huu haujaisha, lakini tayari Simba imeanza kuupamba msimu ujao kwa matumaini, mabadiliko, na ndoto ya kurudi katika ngazi ya fainali Afrika.

Simba imefika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kupoteza mechi mbili tatu katika hatua tofauti, lakini ikilinda rekodi ya kutopoteza mchezo wowote nyumbani, kwani imeshinda sita na kutoka sare moja tu iliyopata juzi kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar dhidi ya Berkane.

SOMA NA HII  SHINDANO LA EXPANSE TOURNAMENT KASINO LINAENDELEA.....!