WINGA Joshua Mutale amekuwa mtamu kama mcharo. Kwa wanaokumbuka wakati anatua Msimbazi kutoka Power Dynamos ya Zambia, jina lake lilibeba matumaini.
Mutale maarufu kama Budo, aliingia kikosi cha Simba kama mmoja wa wachezaji waliotarajiwa kuleta mapinduzi msimu huu, lakini kama ilivyo kwa nyota wengi, safari yake haikuwa tambarare, hata hivyo kwa sasa ni kama gari limewaka na Mzambia huyo amefichua kilichombadilisha na kuwa mtamu nje ndani.
Mutale alipitia kipindi kigumu kilichojaa mashaka, akijikuta nje ya kikosi cha kwanza, huku baadhi ya mashabiki na wadau wakianza kuhoji ubora wake, lakini haikuwa sababu ya kuporomoka zaidi, badala yake, alijikuta akipata nguvu mpya kupitia imani ya kocha Fadlu Davids.
“Wapo mashabiki ambao walikuwa wananitia moyo hata nilipokuwa napitia wakati mgumu. Kocha Fadlu (Davids) na benchi lote la ufundi hawakuwahi kunikatia tamaa. Walinipa sababu ya kupigana, niliamini utafika wakati wangu,” alisema Mutale.
Na kweli, imani hiyo haikuwa bure. Katika wiki chache zilizopita, Budo amekuwa na makali. Aliwasha moto katika mechi za viporo kwenye Ligi Kuu, huku fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane iliyochezwa Zanzibar, akiibuka mchezaji bora wa mechi.
Hata katika fainali ya kwanza huko Morocco, licha ya kuingia dakika ya 80 kuchukua nafasi ya Ellie Mpanzu, alionyesha kitu cha tofauti.
Safari ya Mutale kuuwasha moto haikuanza katika fainali kwani mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji, alichangia mabao mawili ya mwanzo yaliyofungwa na Jean Charles Ahoua akisababisha penalti, jingine akifanyiwa faulo nje ya boksi.
Wakati Simba ikikamilisha viporo vyake dhidi ya KMC, Mutale alitoa asisti mbili zilizomsaidia Steven Mukwala kufunga mabao mawili na kuipa timu hiyo ushindi wa mabao 2-1.
Mchezaji huyo ambaye amejifunga kwa mkataba na Simba hadi 2027, anaonekana sasa kuwa silaha muhimu kwa kocha Fadlu Davids.
Katika hatua ya 16 bora ya Kombe la FA dhidi ya Big Man, Mutale alikuwa mchezaji bora. Kwa wale waliokuwa wakimtazama kwa mashaka, sasa wanalazimika kumtazama kwa heshima wakiamini kweli ana kitu.
Na hata kocha Fadlu hakusita kumwelezea kwa kusema; “Mutale ni mfano wa mchezaji ambaye hakuwahi kukata tamaa. Tulijua muda wake unakuja. Anafanya kazi kwa bidii mazoezini, hana maneno mengi lakini ana njaa ya mafanikio. Tumemlea kwa utulivu, sasa anatupa kile tulichotarajia,” alisema Fadlu.