Pia katika mechi nyingine mbili za Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho (FA), Coastal ilipoteza zote kwa vipigo vya 3-0 na 5-2 mtawalia kuonyesha jamaa walivyo wanyonge mbele ya Azam iliyo na safu kali ya ushambuliaji iliyofunga mabao sita na ukuta mgumu ulioruhusu mabao mawili kupitia mechi tano ilizocheza za Ligi Kuu Bara msimu huu.Coastal yenyewe katika mechi nane imefunga mabao matano tu na kufungwa sita, hali inayoonyesha leo mabeki wa timu hiyo wa kazi ya kuwazuia Japhte Kitambala mwenye bao moja na Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye mabao mawili na asisti moja sambamba na Nassor Saadun mwenye bao moja na asisti mbili alizotoa wakati Azam inaizamisha Simba kwa mabao 2-0 mechi ya mwisho ya Ligi kwa timu hizo.
Hata hivyo, Coastal licha ya kuwa na wastani usioridhisha wa mabao, lakini ina washambuliaji hatari, Athuman Masumbuko ‘Makambo JR’ na Maabad Maulid wenye mabao mawili kila mmoja, lakini ni timu inayotengeneza nafasi kupitia mashambulizi makali kupitia pembeni.
Kwa aina ya soka na mbinu wanazotumia makocha wa timu hiyo, Mohammed Muya na Ibenge ni wazi mashabiki wanatarajia kupata burudani kwenye Uwanja wa Azam Complex, japo wenyeji wana nafasi kubwa ya kuendeleza ubabe kwa Wagosi ambao mara ya mwisho katika Ligi ilipoteza 1-0 kwa watetezi Yanga ikicheza ugenini siku chache baada ya suluhu na Mashujaa mjini Kigoma.
Azam ina faida kubwa ya kikosi hicho kutoka katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ikipoteza klwa penalti 5-4 baada ya kucheza mechi tano mfululizo bila kupoteza ndani ya dakika 90, huku baadhi ya nyota wake wengine kurejea kutoka michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 walipoenda na timu ya taifa, Taifa Stars iliyotolewa hatua ya 16 Bora.
Hata hivyo, kwa mujibu wa makocha wa timu hizo ni kwamba kila mmoja imejiandaa kukabiliana na upinzani wa dakika 90 na itakayotumia vyema dakika hizo ndio itakayoibuka na ushindi.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho Jumapili kwa mechi moja itakayozikutanisha wenyeji Simba dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, huku kila moja ikiwa na kumbukumbu ya matokeo tofauti, Simba ikipoteza mbele ya Azam kwa mabao 2-0, ilihali Wakata Miwa wakitoka suluhu kwenye uwanja huo dhidi ya JKT Tanzania.