Hersi Asalia Bila Mpinzani, Muhula Mwingine Wanukia Yanga
RAIS wa Yanga SC, Eng. Hersi Ally Said, ameweka mguu mmoja mbele kuelekea kuendelea kuiongoza klabu hiyo baada ya kujitokeza akiwa mgombea pekee wa nafasi ya urais kufuatia kukamilika kwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uchaguzi wa viongozi.
Orodha iliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga inaonyesha kuwa hakuna mwanachama mwingine aliyejitokeza kumpa upinzani Hersi, hatua inayompa nafasi kubwa ya kuendelea kuliongoza jahazi la Wananchi kwa muhula mwingine endapo atakidhi vigezo vya mchakato wa uhakiki.
Katika nafasi ya Makamu wa Rais, hali ni kama hiyo baada ya Arafat Ali Haji kuwa mgombea pekee aliyerejesha fomu, huku ushindani mkali ukitarajiwa kwenye nafasi za ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Baadhi ya waliojitosa kuwania nafasi hizo ni Julius John Koyi, Saady Mohammed Khimji, Fredy Stanley Mahembe, Munir Said Seleman, Mshindo Hamza Msolla, Issa Ally Mangungu, Mustapha Salumu Himba na Alexander Francis Ngai, pamoja na wagombea wengine.
Kamati ya Uchaguzi imeeleza kuwa sasa itaanza mchakato wa kuhakiki nyaraka za wagombea wote kabla ya kutangaza orodha rasmi ya watakaoruhusiwa kushiriki uchaguzi.
Iwapo atapitishwa rasmi, Hersi ataendelea kupewa dhamana ya kuiongoza Yanga, huku wanachama na mashabiki wakitarajia uongozi wake kuendeleza mafanikio ya klabu hiyo katika mashindano ya ndani na kimataifa.