Klopp Akipigiwa Chapuo, Nagelsmann akalia kuti kavu Ujeruman
KOCHA wa Ujerumani, Julian Nagelsmann ameanza kukabiliwa na presha ya kibarua chake kuota nyasi baada ya timu yake kutolewa na Paraguay kwa mikwaju ya penalti katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026, huku Jurgen Klopp akiipewa nafasi ya kuchukua nafasi hiyo.
Ujerumani ilitolewa kwa penalti 4-3 baada ya sare ya 1-1 katika dakika 120, matokeo yaliyowakasirisha viongozi wa Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) na mashabiki ambao wamekuwa wakitaka mabadiliko ya haraka kwenye benchi la ufundi.
Klopp ambaye alikuwepo uwanjani Boston kama mchambuzi wa kituo cha Magenta TV, sasa anaongoza kwenye masoko ya ubashiri kupewa jukumu la kuinoa timu hiyo ya taifa.
Baada ya mechi hiyo, Klopp alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuifundisha Ujerumani amesema bado hajafikiria suala hilo.
Kwa upande wake, Nagelsmann amesema hana mpango wa kujiuzulu licha ya presha kubwa inayomkabili.
“Ningependa kuendelea na kazi yangu. Lakini nakubali ukitolewa na Paraguay, huwezi kusema wewe ni timu ya kiwango cha juu tena,” amesema kocha huyo.
Nagelsmann pia amekosoa uamuzi wa mwamuzi kufuta bao la Jonathan Tah kupitia VAR akidai ulikuwa wa utata.
“Kwangu ule ulikuwa uamuzi wa ajabu. Hata hivyo, hatukufanya vya kutosha kushinda. Hatukulinda vizuri na tulikosa utulivu tulipopata nafasi za kushambulia,” ameongeza.
Wengine wameeleza kizazi cha sasa cha wachezaji wa Ujerumani kimeshindwa kurejesha heshima ya taifa hilo tangu kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2014.
Nagelsmann aliteuliwa kuinoa Ujerumani mwezi Septemba 2023 na mwaka 2025 aliongezewa mkataba hadi 2028 lakini baada ya kutolewa mapema kwenye Kombe la Dunia lolote linaweza kutokea.