Vyuma Vitano Mlangoni Arsenal
LONDON, ENGLAND: ARSENAL wanaweza hata kufikia matumizi yao ya rekodi ya Pauni 250 milioni walizotumia kwa ajili ya usajili wa wachezaji katika majira ya joto msimu uliopita, baada ya kuthibitisha usajili wa kudumu wa Pauni 35 milioni wa beki wa kati wa Bayer Leverkusen, Piero Hincapie, wiki hii.
Na baada ya kumshusha Hincapie sasa wanatafuta kuongeza wachezaji wengine watano katika msururu mwingine mkubwa wa matumizi ya majira ya joto ambao kocha Mikel Arteta anadaiwa kuupangalia kwa ufasaha akicheleweshwa tu na fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazoendelea Amerika Kaskazini kwa sasa.
Timu hiyo iliyofika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita imebadilika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa wakati Mikel Arteta alipochukua uongozi wake Desemba 2019, na mabingwa hao wapya wa England wanakusudia kujenga zaidi ubora kutokana na nguvu waliyonayo katika dirisha hili la usajili.
Katika kipindi cha miaka sita na nusu iliyopita, kocha huyo Mhispania ameibadilisha klabu hiyo ya Kaskazini mwa London na baada ya kumaliza nafasi ya pili mara tatu, hatimaye aliwaletea ubingwa wa kwanza baada ya miaka 22, jambo lililosababisha shangwe kubwa ambalo hata kama walipoteza kwa kuumiza na PSG kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Lakini, haya hapa ni majina ya wachezaji wanaolengwa na Arsenal kuja kuendeleza ilipoishia msimu uliopita.
JEREMY MONGA
Arsenal wanamfuatilia mchezaji kinda wa Leicester City, Jeremy Monga, kwa dau la Pauni 10 milioni ambaye licha ya klabu nyingine kadhaa za ligi hiyo kuonyesha nia ya kumsajili, lakini inaaminika Arsenal ndio wanaongoza katika kumnasa winga huyo, 16, kutokana na nia yake ya kuhamia London kaskazini.
The Gunners wanajaribu kufikia makubaliano katika mazungumzo, wakizingatia hali ya mkataba wa mchezaji huyo na nia yake ya kujiunga na klabu hiyo. Monga atasaini mkataba wake wa kwanza wa kitaaluma huko Leicester City ifikapo Julai 10, atakapofikisha miaka 17, hatua itakayowapa uwezo wa kudai ada ya uhamisho kwa ajili ya mchezaji huyo.
TINO LIVRAMENTO
Moja ya malengo makubwa ya Arsenal ni kupata beki wa pembeni mwenye uwezo wa kucheza pande zote mbili za uwanja. Kutokana na historia ya majeraha ya Tino Livramento na thamani kubwa inayotakiwa na Newcastle United, hakuna dalili kubwa kwamba Arsenal watamsajili msimu huu. Hata hivyo, Oscar Mingueza wa Celta de Vigo ya Hispania ni mchezaji anayekidhi mahitaji ya Arteta. Kwa mujibu wa AS, Arsenal wamefahamishwa kuhusu fursa ya kumsajili beki huyo ambaye mkataba wake unamalizika leo, hivyo anaweza kupatikana bure.
Mingueza mwenyewe anataka kuhamia England baada ya kutumia maisha yake yote nchini Hispania.
Akiwa na thamani ya soko ya Pauni 15 milioni, Arsenal wanaweza kupata dili kubwa kwa kumsajili bila kulipa ada ya uhamisho. Mingueza ni mchezaji imara na uwezo wake wa kuepuka majeraha utakuwa wa manufaa makubwa.
CHRISTOS TZOLIS
BBC inaripoti kuwa Arsenal pia mezani wana jina la winga wa Club Brugge ya Ubelgiji, Christos Tzolis, wakitafuta kuboresha safu ya ushambuliaji.
Mapema mwezi huu, ilielezwa kuwa mkurugenzi wa usajili, Andrea Berta, alikuwa akifuata dili hilo, huku Arteta pia akiridhia usajili huo.
Tzolis, 24, anaripotiwa kuwa na hamu kubwa ya kujiunga na Arsenal, jambo linalowapa faida katika harakati za kumsajili. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ugiriki anaweza kupatikana kwa takriban Pauni 35 milioni.
Tzolis, aliyeanzia soka PAOK ya Ugiriki, alifunga mabao matatu katika mechi 30 akiwa Norwich City kati ya 2021 na 2024.
Morgan Rogers ndiye kipaumbele kikuu cha usajili wa Arsenal msimu huu wa joto, lakini dili hilo halitakuwa rahisi kifedha na nyota huyo wa Aston Villa anaonekana kumkosha zaidi Arteta, akiwa na uwezo wa kucheza winga wa kushoto na kiungo. Mchezaji huyo yupo tayari kujiunga na Arsenal licha ya kuvutiwa pia na Manchester United, lakini inaaminika kwamba ada ya zaidi ya Pauni 80 milioni 80 itahitajika ili Villa wafikirie kumuuza staa wao huyo mwenye umri wa miaka 23.
Akizungumza kutoka kambi ya timu ya taifa ya England mapema mwezi huu, Rogers alisema anazingatia zaidi majukumu ya timu ya taifa kuliko uvumi wa uhamisho.
Hata hivyo, ilifichuka wiki iliyopita kuwa kiungo wa Arsenal na England, Declan Rice amekuwa akijaribu kumshawishi kuhamia Emirates.
BRUNO GUIMARAES
Arsenal wanaripotiwa kuandaa ofa ya pili kwa ajili ya kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes baada ya kukataliwa kwa ile ya awali ya Pauni 55 milioni. Ripoti zinaeleza kuwa Arsenal ilikuwa imeshaanza mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo, lakini Newcastle United ilitoa ujumbe kwamba Guimarães hayupo sokoni, baada ya uvumi wa awali kwamba Manchester United pia walikuwa wakimzengea.
Kwa mujibu wa Daily Mail, Arsenal wanajiandaa kurudi na ofa bora kwa ajili ya kiungo huyo wa zamani wa Lyon ambaye amekuwa St. James Park tangu Januari 2022 na ana miaka miwili iliyobaki kwenye mkataba wake.
Tayari amecheza mechi 195 kwa Magpies, akifunga mabao 31 na alisaidia klabu hiyo kuvunja ukame wa mataji kwa kushinda Carabao msimu wa 2024/25.
Newcastle wanaripotiwa kuwa tayari kumpa Guimarães mkataba wa rekodi ya klabu wa Pauni 40 milioni ambao utaongeza mshahara wake hadi takriban Pauni 200,000 kwa wiki na kumfanya abaki hadi 2030.