Nyota Barca Aichomolea Man United
BARCELONA, HISPANIA: MANCHESTER United imepata majibu kuhusu uwezekano wa kiungo chipukizi wa Barcelona, Marc Bernal, kujiunga nayo katika dirisha hili la usajili, baada ya kuikataa timu hiyo.
Barcelona ina kizazi bora cha wachezaji vijana akiwemo Bernal, Lamine Yamal, Pau CubarsI, Gavi na Alejandro Balde ambapo kutokana na changamoto za kifedha katika miaka ya karibuniklabu kadhaa za Ligi Kuu England zimekuwa zikihusishwa na nyota hao.
Kwa mujibu wa Mundo Deportivo, Manchester United, Arsenal na Chelsea zimewasiliana na Barcelona kutaka kujua kama Bernal anaweza kupatikana katika dirisha hili la usajili linaloendelea duniani kote, lakini Bernal mwenyewe amesema “hapana” kwa Manchester United.
Taarifa hiyo inadai Bernal mwenye umri wa miaka 19 ameonyesha uaminifu kwa Barcelona, na ameamua kukataa ofa au mazungumzo kutoka Manchester United, Arsenal na klabu nyingine zinazomtaka. Pia amekuwa akifuatiliwa na AS Roma pamoja na Al-Nassr ambayo ilidaiwa kuwa tayari kumpa mshahara mkubwa zaidi. Licha ya kuvutiwa na klabu hizo, Bernal anataka kubaki Camp Nou nili aendelee kuendelezwa na kocha Hansi Flick.
Baada ya kukosa sehemu kubwa ya msimu wa 2024/25 kutokana na jeraha la goti, mchezaji huyo alirejea msimu uliopita na kufunga mabao matano katika mechi 33 za kikosi cha kwanza.
Mkataba wake una kipengele cha kuvunja kwa Euro 500 milioni, huku Barcelona ikiripotiwa ilikataa ofa ya Euro 30 milioni kutoka Galatasaray mwezi Januari, mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, Manchester United imelazimika kuongeza nguvu kwenye usajili wa kiungo wa West Ham United, Mateus Fernandes.