Straika Simba Atimkia Misri
BAADA ya kuitumikia Simba Queens kwa misimu minne mfululizo, hatimaye mshambuliaji raia wa Kenya, Jentrix Shikangwa, ameondoka ndani ya klabu hiyo akienda kuitumikia FC Masar ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini Misri.
Shikangwa ambaye alijiunga na Simba Queens Septemba 2022 akitokea Vihiga Queens ya Kenya, anaondoka Tanzania akiwa amefunga mabao 69 katika kipindi hicho alichoshiriki Ligi Kuu Soka Wanawake.
Nyota huyo amekuwa mmoja wa wachezaji wa kigeni kucheza Ligi ya Wanawake Tanzania kwa mafanikio makubwa akibeba mataji mawili ya ligi msimu wa 2023-2024 na 2025-2026, taji moja la Cecafa sawa na Ngao ya jamii, pia kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake msimu wa 2023-2024.
Inaelezwa Masar ambayo ni bingwa wa Ligi ya Wanawake Misri, imeweka ofa nono kiasi cha kumng’oa nyota huyo kikosini hapo kwani awali hakuwa na mpango wa kuondoka.
Tayari mshambuliaji huyo amewasili nchini Misri kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usajili wake ambao unaelezwa Simba Queens imeridhia nyota huyo kuondoka.
“Baada ya kuwa na msimu mzuri, Masar imevutiwa naye na viongozi wa Simba wameridhia Shikangwa akatafute changamoto mpya, hivyo tayari wameanza mchakato wa kutafuta mbadala wake,” kilisema chanzo cha ndani.
Kupitia chapisho lake katika mitandao ya kijamii, Simba imetoa taarifa juu ya kuondoka kwa Shikangwa ikiandika: “Asante kwa sanaa yako ya kucheka na nyavu, kumbukumbu tunazo nyingi. Asante Jentrix Shikangwa.”
Kuondoka kwa Shikangwa, ni muendelezo wa Simba Queens kuuza wachezaji nje ya nchi licha ya kwamba bado wanahitajika ndani ya timu kutokana na kiwango bora. Wengine waliowahi kuuzwa nje na klabu hiyo ni Opah Clement, Julietha Singano na Vaileth Nickolaus.
Kwa kutua kwake Misri, Shikangwa anaungana na Watanzania Hasnath Ubamba ambaye yuko kikosini hapo kwa takribani msimu wa tatu pamoja na Vaileth Nickolaus aliyetolewa kwa mkopo.
Shikangwa amekuwa na kiwango bora tangu atue Simba Queens, msimu wake wa kwanza 2022-2023 aliibuka mfungaji bora wa ligi akiweka kambani mabao 17.
Uliofuata 2023-2024 alifunga mabao 12 kwenye mechi 10 za mashindano yote, kisha msimu wa 2024-2025 akafunga mabao 24 akimaliza nyuma ya Stumai Abdallah wa JKT Queens aliyeibuka mfungaji bora Ligi Kuu Wanawake kwa mabao 28.
Msimu huu wa 2025-2026, amekuwa na muendelezo bora wa kupachika mabao akiweka nyavuni 16 na kuisaidia Simba Queens kurejea kwenye mashindano ya kimataifa kufuatia kutwaa ubingwa wa ligi.
Kwa takwimu na mchango wake ndani ya misimu minne, wengi wanaamini Shikangwa anaondoka akiwa ndiye mshambuliaji bora wa kigeni kuwahi kucheza Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, huku namba zake zikiendelea kuzungumza kuliko maneno.
Akizungumza na Soka la Bongo, Shikangwa amesema: “Nitapamisi sana Tanzania kwani wamenionyesha upendo mkubwa sana tangu nafika msimu wangu wa kwanza.”