Mkenya Presha Yaanza Mtibwa Sugar
KICHAPO cha mabao 2-1 ilichokipata Mtibwa Sugar dhidi ya Tanzania Prisons, kimemfanya kocha mkuu wa kikosi hicho, Mkenya, Yusuf Chippo kusema anahitaji miujiza zaidi ya kuinusuru timu hiyo katika kuepuka kushuka daraja.
“Mechi yetu na Namungo ndiyo itakayotupa taswira ya tutakachokipata, ni hatua ngumu sana kwetu kwa sababu hayakuwa malengo kuona timu inakuwa katika nafasi ya presha kubwa kama ilivyokuwa sasa, kiukweli inaniumiza,” amesema Chippo.
Kocha huyo amesema timu hiyo ilianza vizuri msimu lakini bahati mbaya mambo yalibadilika ghafla, hasa baada ya kutumia mechi zao nyingi za nyumbani kwenye viwanja vya nje ya Morogoro jambo lililosababisha kukosa mashabiki halisi wa kikosi hicho.
Katika mechi 29 ilizocheza Mtibwa Sugar, imeshinda sita, sare tisa na kupoteza 14, ikishika nafasi ya 15 na pointi 27, ikihitaji miujiza kujinasua kushuka daraja, kuungana na KMC FC iliyoshuka tayari ikiwa ya 16 na pointi tisa.
Ni mechi mbili pekee ambazo Mtibwa imecheza Morogoro msimu huu dhidi ya KMC na Simba baada ya Uwanja wa Jamhuri kufungiwa kwa muda mrefu, huku ikiifanya timu hiyo mechi zake za nyumbani kutumia viwanja tofauti ikiwemo Uwanja wa KMC Complex uliopo Dar es Salaam, Jamhuri (Dodoma) na Airtel (Singida).
Ikiwa Mtibwa Sugar itatoka sare ya aina yoyote au kupoteza dhidi ya Namungo katika mechi ya kesho Jumanne, itashuka daraja moja kwa moja na kuiachia Prisons iliyo nafasi ya 14 na pointi 29, kujihakikishia kucheza Play-Off (mtoano), ili kujinasua kutoshuka.